Rouhani asema mahudhurio makubwa yataimarisha izza, usalama wa Iran
Rais Hassan Rouhani wa Iran ametoa wito kwa wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa rais unaofanyika hii leo hapa nchini akisisitiza kuwa, mahudhurio makubwa katika zoezi hilo yataimarisha izza na usalama wa Jamhuri ya Kiislamu.
Dakta Rouhani ambaye anagombea kiti cha rais kwa muhula wa pili ameyasema hayo baada ya kupiga kura yake mapema asubuhi na kuongeza kuwa, wananchi wa Iran wataamua mustakabali wa taifa lao kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huu.
Amefafanua kuwa, mahudhurio makubwa yatafungua njia ya maendeleo-endelevu kwa nchi hii, hususan katika kipindi hiki ambapo Iran inakaribia kuingia katika karne mpya, kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani.
Kadhalika amebainisha kuwa, uchaguzi huu una umuhimu mkubwa kwani utaathiri moja kwa moja nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kieneo na kimataifa.
Awali Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia aliwataka wananchi wa Iran kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa leo wa rais unaofanyika sambamba na duru ya tano ya uchaguzi wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji na uchaguzi mdogo wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).
Wakati huo huo, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini amesema anafuatilia kwa karibu na heshima kubwa uchaguzi wa leo wa Iran akisisitiza kuwa EU kama ilivyofanya huko nyuma, itashirikiana na shakhsia yeyote atakachaguliwa na wananchi.
Mbali na uchaguzi huo kuendelea hapa nchini, raia wa Iran wanaoishi nje ya nchi pia wanashiriki zoezi hilo katika nchi za Indonesia, Australia, New Zealand, Lebanon, Russia, Kuwait na Japan miongoni mwa nchi nyingine 102 kote duniani.