Rouhani: Iran kuendeleza ushirikiano wa pande tatu na Russia, Syria
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendeleza ushirikiano na Russia katika kuimarisha amani, uthabiti na mapambano dhidi ya ugaidi hasa nchini Syria.
Rais wa Iran Hassan Rouhani ameyasema hayo leo Jumamosi katika mazungumzo ya simu na Rais Vladimir Putin wa Russia. Katika mazungumzo hayo, Rouhani ametangaza kuunga mkono ushurikiano wa pande tatu wa Iran, Russia na Uturuki katika kudumisha usitishwaji mapigano Syria.
Rouhani amesema baadhi ya nchi kama vile Marekani na Saudia zinapelekea hali kuwa mbaya zaidi katika eneo. Amesema nchi zote zinapaswa kuwa na muungano wa kweli wa kupambana na ugaidi ili kuleta uthabiti katika eneo.
Rais Rouhani hali kadhalika amesema Iran inafungamana na utekelezaji wa mapatano ya nyuklia iliyofika na madola sita makubwa duniani.
Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin amempongeza Rais Hassan Rouhani kwa ushindi wake katika uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni nchini Iran. Amesema Russia na Iran ziko nchini Syria kufuatia mwaliko wa serikali halali ya nchi hiyo na kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Ametaka pia Tehran na Moscow ziendeleze ushirikiano kwa ajili ya kuimarisha amani na uthabiti nchini Syria na eneo zima la Asia Magharibi.