Meli za Kivita za Iran kuelekea Bahari ya Hindi kulinda doria
Msafara wa meli za kivita za Iran zinatazamiwa kuelekea katika Bahari ya Hindi mwezi ujao kulinda doria na kusindikiza meli za mafuta na za kibiashara za Iran.
Msafara wa 47 wa Manowari za Iran unatazamiwa kuelekea katika Bahari ya Hindi mapema mwezi Juni, amedokeza Naibu Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran Admeri Peyman Ja'fari Tehrani.
Akizungumza Jumamosi amesema, "Msafara wa 46 wa Manowari za Iran umekuwa katika maji ya kimataifa kwa muda sasa na unatarajiwa kurejea nchini Iran katika kipindi cha siku chache zijazo."
Kamanda huyo amesema meli za kivita za Iran zina jukumu la kulinda usalama wa meli za mafuta na kibiashara za Iran zilizo katika maji ya kimataifa hasa Ghuba ya Aden, Lango Bahari la Bab el-Mandeb na Bahari ya Hindi. Msafara huo 46 wa meli za kivita za Jeshi la Wanamaji la Iran pia una majukumu ya kufanya upelelezi na kutekeleza oparesheni baharini na unajumuisha manowari mbili za Sabalan na Lavan.
Katika miaka ya hivi karibuni, Jeshi la Majini la Iran limeimarisha harakati zake katika maji ya kimataifa kwa lengo la kudumisha usalama na kulinda meli za kibiashara na zinazobeba mafuta. Wanamaji wa Iran wamefanikiwa pakubwa kuzuia hujuma nyingi za maharamia wanaolenga kuteka meli za Iran na za mataifa mengine katika maji ya kimataifa.
Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran Admeri Habibullah Sayari anasema kutumwa meli za kivita za Iran katika maji ya kimataifa ni ishara ya nguvu na uwezo wa Iran mbele ya maadui.