Iran itatoa jibu kali kwa magaidi wanaopania kufanya mashambulizi nchini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30754-iran_itatoa_jibu_kali_kwa_magaidi_wanaopania_kufanya_mashambulizi_nchini
Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa jibu kali zaidi kwa magenge ya kigaidi yatakayojaribu kuleta chokochoko na kufanya mashambulizi ndani ya ardhi ya nchi hii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2017 23:34 UTC
  • Iran itatoa jibu kali kwa magaidi wanaopania kufanya mashambulizi nchini

Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa jibu kali zaidi kwa magenge ya kigaidi yatakayojaribu kuleta chokochoko na kufanya mashambulizi ndani ya ardhi ya nchi hii.

Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumanne hapa mjini Tehran akiashiria shambulizi la kombora lililofanywa hivi karibuni na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC dhidi ya ngome za kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh huko Dayr al-Zawr nchini Syria.

Amesema makombora ya masafa ya kati ya ardhi kwa ardhi yaliyotumiwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika shambulizi hilo yana usahihi mkubwa; na kwamba uamuzi wa kushambulia ngome za Daesh huko Syria haukupasishwa na mtu au taasisi moja hapa nchini, bali ulipata baraka kamili za Baraza Kuu la Usalama wa Taifa (SNSC).

Jumapili iliyopita, zaidi ya magaidi 65 wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) waliangamizwa baada ya kombora moja kati ya sita ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kulenga kamandi ya kijeshi ya kundi hilo katika mji wa Al-Mayadin ulioko kwenye viunga vya Deir Ezzor mashariki mwa Syria.

Kombora la Iran likielekea kuwaangamiza magaidi wa Desh Syria

Hujuma hii ya Iran ni jibu kwa jinai ya kigaidi iliyofanywa tarehe 7 ya mwezi huu wa Juni hapa mjini Tehran katika ofisi za Bunge la Iran na Haram ya Imam Khomeini (MA) na kusababisha kuuawa shahidi watu 18 na kujeruhiwa wengine 52.

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesisitiza kuwa, hujuma hiyo dhidi ya Tehran ya Juni 7 haikuwa ya kwanza dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kufafanua kuwa, Wizara ya Intelijensia kwa ushirikiano na Majeshi ya Iran zimefanikiwa kutibua majaribio kadhaa ya mashambulizi ya kigaidi ndani ya ardhi ya Iran.