Iran kuendelea kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30758-iran_kuendelea_kuimarisha_uhusiano_wake_na_nchi_za_afrika
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesisitiza kuwa, ni katika sera zilizo madhubuti za nchi hii kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 21, 2017 03:00 UTC
  • Iran kuendelea kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesisitiza kuwa, ni katika sera zilizo madhubuti za nchi hii kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika.

Rais Rouhani aliyasema hayo jana hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Naim Akibo, balozi mpya wa Benin hapa nchini na kuongeza kuwa, Iran na nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika zina fursa nzuri ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbali mbali.

Amesema changamoto ambazo zimekuwa zikilikabili eneo la Mashariki ya Kati katika miaka ya hivi karibuni, zimekuwa na taathira za moja kwa moja kwa bara muhimu la Afrika; hususan suala la uingiliaji wa masuala ya ndani wa madola ya kibeberu na zimwi la ugaidi na misimamo ya kufurutu ada.

Rais Rouhani na baadhi ya wanadiplomasia wa Benin

Dakta Rouhani amesema changamoto zinazoyakabili maeneo hayo mawili ya kistratajia (Afrika na Mashariki ya Kati) hazina suluhu nyingine isipokuwa mazungumzo ya kisiasa.

Kwa upande wake, balozi mpya wa Benin mjini Tehran amempongeza Rais wa Iran kwa jitihada zake za kupatia ufumbuzi matatizo ya kieneo kwa lengo la kurejesha uthabiti katika kanda hii.

Mbali na mwanadiplomasia huyo wa Benin, Naim Akibo, Rais Rouhani jana aliwapokea mabalozi wengine wapya wa nchi kadhaa zikiwemo za Malaysia na Mexico.