Rais Rouhani: Matatizo ya mazingira yatatuliwe kimataifa
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ulindaji mazingira ni dharura kwa ajili ya afya, ustawi na kuzuia kuhajiri watu kutoka maeneo yao.
Aidha amesisitiza kuwa, utatuzi wa tatizo la mazingira ni jambo linalohitaji uwekezaji, mikakati maalumu na ushirikiano wa kieneo na kimataifa.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo Jumatatu mjini Tehran katika mkutano wa kimataifa wa "Kukabiliana na Kimbunga cha Mchanga, Changamoto na Njia za Kivitendo za Utatuzi." Ameongeza kuwa, asilimia 80 ya kimbunga cha mchanga nchini Iran hutokana na uharibifu wa mazingira katika nchi za Iraq, Jordan, Kuwait, Syria, Saudi Arabia, Pakistan, Afghanistan na Turkmenistan.
Kwingineko, katika hotuba yake, Rais Rouhani amesema, ugaidi ni sumu ambayo imeteka eneo lote la Mashariki ya Kati na kwamba tawala zote zinazotumia ugaidi kufikia malengo haramu zifahamau ugaidi pia utazisibu.
Wakati huo huo mshauri wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza katika kongamano hilo, ameipongeza Iran kwa hatua ilizochukua kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.