Zarif: Iran haitasahau jinai ya Marekani ya kutungua ndege ya abiria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i31300-zarif_iran_haitasahau_jinai_ya_marekani_ya_kutungua_ndege_ya_abiria
Waziri wa Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran kamwe haitasahau jinai ya Marekani ya kutungua ndege yake ya abiria katika Ghuba ya Uajemi.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jul 03, 2017 23:06 UTC
  • Zarif: Iran haitasahau jinai ya Marekani ya kutungua ndege ya abiria

Waziri wa Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran kamwe haitasahau jinai ya Marekani ya kutungua ndege yake ya abiria katika Ghuba ya Uajemi.

Zarif ameyasema hayo  kwa mnasaba wa kumbukumbu ya hatua ya meli ya kivita ya Marekani kutungua ndege ya abiria ya  Iran Air Julai 3 mwaka 1988. Katika ujumbe alioutuma Jumatatu usiku kupitia akaunti yake ya Twitter, Zarif amebainisha masikitiko yake kuwa, wakuu wa Marekani walizidisha ukatili wao huo pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho cha kuwaua raia na kwa hiyo watu wa Iran kamwe hawatasahau jinai hiyo.

Ndege ya abiria ya Iran ilitunguliwa na Marekani katika jinai ya kuogofya

Ikumbukwe kuwa, miaka 29 iliyopita  ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege la Iran Air iliyokuwa ikitokea mji wa Bandar Abbas, kusini mwa Iran kuelekea Dubai, ilishambuliwa kwa makombora mawili ya jeshi la Marekani kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo. Kati ya abiria waliokuwa katika ndege hiyo ni watoto 66, wanawake 53 na raia 46 wa nchi zingine duniani.

Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama na ugaidi unaotekelezwa na serikali ya Marekani. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao huo pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho cha kigaidi.