Iran: Kamwe hatutoacha kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i31364-iran_kamwe_hatutoacha_kuwaunga_mkono_wananchi_wanaodhulumiwa_wa_palestina
Msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) anayehusika na masuala ya kimataifa alisema jana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitaacha kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
(last modified 2026-09-23T04:25:36+00:00 )
Jul 05, 2017 03:46 UTC
  • Iran: Kamwe hatutoacha kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina

Msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) anayehusika na masuala ya kimataifa alisema jana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitaacha kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.

Hossein Amir Abdollahiyan alisema hayo jana wakati alipoonana na Nicholas Kitty Kitty, balozi wa Zimbabwe hapa mjini Tehran na kusema kuwa kuna udharura wa nchi huru duniani kulipa umuhimu mkubwa suala la kuwaunga mkono na kuwasaidia wananchi madhlumu wa Palestina.

Aidha amesema, kitendo cha Marekani cha kutumia vibaya maneno kama haki za binadamu kuziwekea vikwazo nchi nyingine huru duniani kinaonesha kuwa Washington inaendesha siasa hizo za dhulma ili kuzishinikiza nchi huru na zisizokubali kuburuzwa duniani.

Wapalestina katika maziko ya shahid aliyouliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Msaidizi huyo maalumu wa Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa, uhusiano wa Iran na Zimbabwe ni mzuri na unazidi kustawi. Amesema, Iran na Zimbabwe zinapaswa kutumia vizuri uwezo na nafasi ya kisiasa, kiuchumi, kibiashara, kiafya na kimatibabu katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili kadiri inavyowezekana.

Kwa upande wake, balozi wa Zimbabwe hapa mjini Tehran, Nicholas Kitty Kitty amesema katika mazungumzo hayo kwamba nchi yake iko tayari kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga zote. Amesema, Harare ina hamu ya kuona uhusiano wake na Tehran unaimarika kadiri inavyowezekana.

Amesema, hatua ya Zimbabwe ya kurahisisha sana kutoa viza kwa raia wa Iran kwa ajili ya kutembelea nchi hiyo inaonesha namna Harare inavyoupa umuhimu mkubwa uhusiano wake na Tehran.