Rais Rouhani aomboleza kifo cha mwanahisabati bingwa wa Iran na dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i31810-rais_rouhani_aomboleza_kifo_cha_mwanahisabati_bingwa_wa_iran_na_dunia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Maryam Mirzakhani, mwanahisabati bingwa na mwenye kipawa che kipekee wa Iran na dunia.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jul 15, 2017 08:36 UTC
  • Rais Rouhani aomboleza kifo cha mwanahisabati bingwa wa Iran na dunia

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Maryam Mirzakhani, mwanahisabati bingwa na mwenye kipawa che kipekee wa Iran na dunia.

Maryam Mirzakhani ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza na pia Muirani wa kwanza kupata Tuzo ya Fields Medal, ambayo ni zawadi bora zaidi ya utafiti wa hesabu duniani, amefariki leo akiwa na umri wa miaka 40 baada ya kuugua saratani ya matiti kwa muda wa miaka minne. Katika ujumbe wake, Rais Rouhani ameandika kuwa: "Kutia fora kusiko na kifani msomi huyo mbunifu na mwanadamu mnyenyekevu kumeinua jina la Iran katika ulimwengu wa elimu." Ameongeza kuwa alikuwa na nafasi ya juu katika kuwaarifisha wanawake Wairani kuelekea katika kilele cha kupata fahari kimataifa katika nyuga mbali mbali. Rais Rouhani amesema Bi. Mirzakhani ameacha athari za kudumu na ameitakia familia yake subira katika kipindi hiki kigumu.

Bi Maryam Mirzakhani enzi za uhai wake

Wengine waliotuma salamu za rambi rambi ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif, Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran Ali Akbar Salehi, Waziri wa Elimu Mohamad Farhadi na Gary Lewis Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Iran. Maryam Mirzakhani alizaliwa mjini Tehran mwaka 1977 na alipata shahda ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Shariff mjini Tehran na kisha akaendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani na mwaka 1999 akiwa mhadhiri na mtafiti katika  Chuo Kikuu cha Princeton alifanikiwa kutatua tatizo sugu la hisabati. Mbali na Tuzo ya Fields Medal kati ya tuzo zingine alizopata ni kutambuliwa na jarida la Popular Science kuwa kati ya wasomi bora zaidi wa mwaka.

Maryam Mirzakhani, mwanamke wa kwanza kushinda tunzo ya Nobel ya Hisabati