Iran na Uganda zasisitiza kukuza zaidi ushirikiano baina yao
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uganda zimesisitiza juu ya kustawisha zaidi ushirikiano baina yao katika nyanja mbalimbali.
Hayo yamesisitizwa katika mazungumzo baina ya balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kampala, Uganda na Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu na kueleza azma ya nchi zao ya kukuza zaidi ushirikiano katika nyuga mbalimbali.
Katika mazungumzo yao hayo mjini Kampala, Jenerali Moses Ali, Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu wa Uganda na Sayyid Murteza Murtazavi balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kampala wameelezea udharura wa kuchukuliwa hatua zaidi za kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika masuala tofauti hususan ya kiuchumi, kilimo, mipango ya ujenzi na nishati.
Aidha wawili hao sambamba na kujadili matukio ya Mashariki ya Kati (magharibi mwa Asia) wamesisitiza juu ya kuweko mapambano na vita vya kweli dhidi ya ugaidi na kudumishwa umoja na udugu miongoni mwa nchi za Kiislamu.
Balozi wa Iran mjini Kampala ameashiria ushiriki wa asilimia 73 wa wananchi wa Iran katika uchaguzi uliopita wa Rais na kuwaalika maafisa wa ngazi za juu wa Uganda kuja mjini Tehran kwa ajili ya kushiriki katika sherehe za kuapishwa Rais Hassan Rouhani zitakazofanyika Agosti 5 ya mwezi ujao.
Kwa upande wake Jenerali Moses Ali, Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu wa Uganda amebainisha kwamba, nchi yake imeazimia kukuza uhusiano na ushirikiano wake na Iran hususan katika masuala ya kiuchumi.