Rais Rouhani: Iran haitokubali njama za maadui za kutaka itengwe kwa nguvu
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa pamoja na kwamba taifa hili limelipa na linaendelea kulipa gharma kutokana na azma yake ya kuwa na izza ya kujitegemea, lakini kamwe mfumo tawala wa nchi hii hautakubali njama za maadui za kutaka itengwe kwa nguvu.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo Alkhamisi ya leo baada ya kuidhinishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei kuwa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kuwa, Iran haitosalimu amri kwa matakwa ya wasiotakia mema kwamba isishiriki kikamilifu katika shughuli za mfumo wa kimataifa kama ambavyo pia haitoridhia kubakia nyuma katika mabadiliko na mafanikio yaliyopatikana kwa tajriba ya mwanadamu.
Sambamba na kubainisha kwamba, makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA yalionyesha ni namna gani Iran ya Kiislamu ilivyo na nia njema kwa ajili ya kuamiliana kwake katika ngazi ya kimataifa, Rais Hassan Rouhani ameongeza kuwa, hii leo taifa la Iran linajiamini zaidi ya ilivyokuwa huko nyuma; na kwa uungaji mkono wa wananchi lilishuhudia uchaguzi wa hamasa wa tarehe 19 Mei mwaka huu na hivyo kuthibitisha nafasi yake athirifu duniani kupitia fremu ya katiba. Akiashiria kuwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran unategemea kura za wananchi amesema kuwa, kujitokeza kwa wananchi kunaufanya Mfumo wa Kiislamu nchini usikumbwe na mkwamo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya 12 imewasilisha mpango wake wa kiuchumi juu ya siasa jumla za mfumo na uchumi wa kimapambano na kuongeza kuwa, serikali ya Iran inakusudia kuleta mapinduzi ya kiuchumi. Sherehe ya kuidhinisha kura za wananchi kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu zimefanyika leo asubuhi katika Husseiniya ya Imamu Khomeini (M.A) hapa Tehran kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kumuidhinisha Hassan Rouhani kuwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.