Rais Mugabe awasili Tehran kuhudhuria sherehe ya kuapishwa Rais Hassan Rouhani
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amewasili hapa mjini Tehran kuhudhuria sherehe ya kuapishwa Rais Hassan Rouhan itakayofanyika Jumamosi ya kesho.
Rais Mugabe amewasili mjini Tehran akiongoza ujumbe wa nchi yake huku viongozi wa mataifa mbalimbali wakiendelea pia kuwasili hapa nchini kwa ajili ya kuhudhuria hafla hiyo. Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassem na Ramadhan Abdullah Shallah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Jihadul Islam ya Palestina nao waliwasili asubuhi ya leo kwa ajili ya kuhudhuria sherehe ya kuapishwa Rais Rouhani.
Viongozi na wawakilishi wa nchi kama Sierra Leone, Guinea, Suriname, Hungary na wawakilishi wa Uingereza na Ureno, Makamu wa Rais wa Ireland, Naibu Spika wa Bunge la Niger ni miongoni mwa wageni waliowasili hapa nchini hii leo kwa ajili ya kuhudhuria sherehe hiyo.
Aidha tayari makumi ya viongozi na wawakilishi wa nchi nyingine za dunia wamewasili mjini Tehran kwa ajili ya shughuli hiyo. Tanzania inawakilishwa na Spika wa Bunge Job Ndugai ambaye tayari amewasili mjini Tehran.
Hassan Rouhani ambaye alichaguliwa tena kuwa Rais wa Iran katika duru ya 12 ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliofanyika Mei 19 mwaka huu kwa kupata kura zaidi ya milioni 23, aliidhinishwa jana na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa Rais wa Iran kwa kipindi kingine cha miaka minne.
Viongozi na wawakilishi wa karibu nchi mia moja wanatarajiwa kuhudhuriwa sherehe ya kuapishwa rasmi Hassan Rouhani katika ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Tehran.