Rouhani aapishwa kuwa rais wa 7 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Dakta Hassan Rouhani jioni ya leo amekula kiapo cha kuwa rais wa 7 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kipindi kingine cha miaka minne kwa kuahidi mbele ya Qur'ani tukufu kwamba atalinda Uislamu, Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na Katiba ya nchi.
Rais Hassan Rouhani amekula kiapo hicho mbele ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani katika sherehe iliyofanyika katika ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu na kuhudhuriwa na Mkuu wa Idara ya Mahakama, Ayatullah Sadiq Amoli Larijani, wawakilishi wa Bunge, wanachama wa Baraza la Kulinda Katiba na wageni waalikwa kutoka nje ya nchi.
"Nitalinda dini rasmi ya nchi hii, Utawala wa Jamhuri ya Kiislamu na Katiba ya Iran, na nitatumia nguvu na mamlaka yangu katika kutekeleza majukumu niliyopewa na kujisabilia kwa ajili ya kuhudumia wananchi, kustawisha nchi, kueneza dini na maadili, kuunga mkono haki na uadilifu, na kujiepusha na udikteta. Nitatetea uhuru na heshima za watu na haki za taifa zilizoainishwa na Katiba", amesema Rais Rouhani wakati anaapisha bungeni.
Baada ya kuapishwa rasmi, Rais Rouhani alitia saini hati ya kiapo mbele ya Mkuu wa Idara ya Mahakama hapa nchini na wajumbe wa Baraza la Kulinda Katiba.
Sherehe za kuapishwa Rais Rouhani zimehudhuriwa na marais, maspika wa mabunge, mawaziri wakuu, mawaziri wa nchi za nje, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Uyala na wawakilishi wa zaidi ya nchi mia moja.