Iran, muungaji mkono wa umoja na kulindwa ardhi yote ya Iraq
Sambamba na familia ya Masoud Barzani kushikilia iitishwe kura ya maoni katika eneo la Kurdistan nchini Iraq, maulama na shakhsia wa kidini pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo wamekutana na viongozi wa Iran hapa mjini Tehran na kujadili matukio yanayojiri hivi sasa nchini Iraq.
Katika kikao hicho na maulama na viongozi wa Iraq cha kujadili suala la kura ya maoni ya eneo la Kurdistan, Ali Akbar Velayati, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa alisisitiza kuwa, taifa la Iran linaunga mkono umoja na kulindwa ardhi yote ya Iraq kama ambavyo pia inapinga aina yoyote ya ukusanyaji maoni kwa lengo la kuyatenganisha baadhi ya maeneo na ardhi yote ya nchi hiyo. Sambamba na kubainisha kwamba takwa la upande wowote la kutaka kujitenga linakinzana na maslahi ya kitaifa ya Iraq, Velayati aliwahutubu shakhsia hao wakubwa wa taifa hilo kwa kusema, suala hilo litapelekea kuigawa Iraq na hakuna shaka kwamba Wairaq nao watasimama kukabiliana nalo.
Wakati huo huo, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iraq, Yan Kubish Jumatatu iliyopita alikutana na Hossein Amir-Abdollahian, Msaidizi Maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa na kubadilishana naye mawazo kuhusiana na suala la usalama na amani ya Iraq. Hii ni kusema kuwa, masuala kama 'usalama' 'uthabiti' na 'kulindwa umoja wa ardhi yote ya Iraq' daima yamekuwa yakisisitiziwa sana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Siasa za Iran kuzihusu nchi majirani na za eneo, zimekuwa ni za kutaka kujitawala na pia kupinga aina yoyote ya kuzigawa nchi hizo. Siasa hizo za Tehran zinabainika wazi katika suala zima la Iraq.
Wakati usalama wa Iraq ulipokuwa hatarini kufuatia nchi hiyo kuvamiwa na genge la kigaidi la Daesh (ISIS), Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilichukua hatua haraka za kuzisaidia serikali za Baghdad na Erbil kukabiliana na kundi hilo. Katika suala la usalama, Iran ilitumia uwezo wake kuisaidia Iraq na kuzuia wanachama wa kundi hilo hatari kufika katika miji ya Baghdad na Erbil. Hivi sasa pia na baada ya kuangamizwa na kufurushwa wanachama wa kundi hilo kutoka mji wa Mosul, uliokuwa makao makuu yao, siasa za Iran ya Kiislamu zimeendelea kuwa zilezile za kusisitizia udharura wa kulindwa umoja wa ardhi yote ya Iraq. Lengo la fitina za Daesh nchini Iraq lilikuwa ni kusambaratisha umoja wa kitaifa wa nchi hiyo, hata hivyo njama hizo zilifelishwa na uelewa mkubwa wa viongozi wa kidini, raia na makundi tofauti ya taifa hilo.
Ukweli ni kwamba kipindi cha baada ya Daesh ni kipindi kigumu na nyeti sana na ambacho pia kinahitaji uelewa wa hali ya juu wa Wairaq hususan maulama wa nchi hiyo. Siasa za kuzidhoofisha nchi za Kiislamu na zenye kujitegemea katika eneo la Mashariki ya Kati zimekuwa zikitekelezwa kwa njia tofauti na maadui hususan utawala wa Kizayuni wa Israel ambapo katika hilo hutumia uungaji mkono kwa pande fulani ndani ya mataifa hayo lengo kuu likiwa ni kuzigawa nchi hizo na kuzitoa kwenye mstari wake. Hata hivyo mara zote njama hizo zimekuwa zikiishia kufeli. Pendekezo la familia ya Masoud Barzani la kutaka iitishwe kura ya maoni kwa ajili ya kujitenga eneo la Kurdistan, halina mustakabali mwema kwa Wakurdi wa eneo hilo na pia si kwa maslahi ya usalama na amani ya eneo na hata kwa Iraq yenyewe.
Katika uwanja huo, Ibrahim al-Jaafari Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq katika kikao na wawakilishi wa chama cha Demokrasia cha Kurdistan (Democratic Party of Kurdistan) wanaoliwakilisha eneo hilo katika bunge la Iraq alisema, nchi zote zinaamini kwamba umoja wa Iraq kwa ajili ya usalama wa eneo ni suala muhimu na Iraq inatumia uwezo wake wote kuziunganisha pande zote na makundi tofauti ya kisiasa kupitia njia ya mazungumzo. Hivi sasa ongezeko la upinzani katika ngazi ya kitaifa, kieneo na kimataifa linazidi kushuhudiwa kuhusiana na sisitizo la Masoud Barzani la kutaka kuitisha kura ya maoni. Kuhusiana na suala hilo, Jumanne iliyopita, Shirika la Habari la Kurdpress lilimnukuu Rabun Maroof, msemaji wa harakati za kupinga kura ya maoni ya eneo hilo akisema: "Tunaamini kuwa kura hiyo ya maoni haitakuwa na maslahi yoyote kwa malengo na madhumuni ya Wakurdi."