Hatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Tuhesabu nafsi zetu kabla ya kuhesabiwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i33006-hatibu_wa_swala_ya_ijumaa_tehran_tuhesabu_nafsi_zetu_kabla_ya_kuhesabiwa
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amewataka waumini kuhesabu nafsi zao kabla ya kuhesabiwa Siku ya Kiyama.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 11, 2017 11:43 UTC

Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amewataka waumini kuhesabu nafsi zao kabla ya kuhesabiwa Siku ya Kiyama.

Ayatullah Muhammad Ali Muvahhedi Kermani amezungumzia umuhimu wa Maadi na Siku ya Malipo na kusema kuwa, moja kati ya sifa za siku hiyo ni kuhesabiwa amali na matendo ya waja waliyoyafanya hapa duniani. Amesema, katika siku hiyo amali na matendo yote ya waja yatashughulikiwa na kuhesabiwa na amewataka waumini kuchunga matendo na mienendo yao. 

Akisisitiza umuhimu wa kuhesabu matendo na amali zetu kabla ya kuhesabiwa mbele ya Mola Muumba Siku ya Kiyama, hatibu wa Swala ya leo ya Ijumaa mjini Tehran amesema: Katika siku hiyo hisabu za baadhi ya wanadamu zitakuwa ngumu na nzito na za wengine zitakuwa nyepesi na sahali na kwamba, yote hayo yanategemea amali na matendo ya mja hapa duniani. 

Swala ya Ijumaa Tehran

Ayatullah Kermani ameashiria aya za Qur'ani tukufu zinazozungumzia masaibu na hali ya kutisha ya Siku ya Kiyama na kuwahimiza waumini kuchunga matendo na mienendo yao. Amesema, kwa mujibu wa aya za Qur'ani tukufu na hadithi za Mtume Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu, Waislamu wote wanapaswa kuwa macho na makini kuhusu matendo na mienendo yao hapa duniani ili wasipatwe na madhara na hasara katika ulimwengu wa Akhera.