Rouhani: Marekani ikituwekea vikwazo vipya, tutatumia masaa kujiondoa JCPOA
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itatumia masaa machache kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Vienna, iwapo Marekani itathubutu kuliwekea taifa hili vikwazo vipya.
Rais Rouhani aliyasema hayo leo katika kikao cha wazi cha Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) cha kujadili majina ya baraza jipya la mawaziri.
Dakta Rouhani amesema kitendo cha Marekani kuiwekea vikwazo Iran ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama JCPOA na kwamba iwapo Washington inataka mchezo huo, basi Iran ina uwezo wa kujiondoa kwenye makubaliano hayo kwa kutumia masaa na wala sio wiki au mwezi.
Amesema: "Wale wanaotaka kutumia lugha ya vikwazo, wamenaswa katika mtego wa njozi za huko nyuma, hivyo iwapo Marekani itazidi kuisukuma ukutani Iran, basi walimwengu watajionea wenyewe namna Iran ilivyofanikiwa katika kurejesha haki zake kwa upande mmoja, na namna Marekani ilivyofeli katika kushinikiza matakwa yake."
Makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi wanachama wa kundi la 5+1 maarufu kwa kifupi kama (JCPOA) ni mwafaka uliopasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Julai mwaka 2015 baada ya kusainiwa na nchi husika katika mazungumzo ya nyuklia na kuanza kutekelezwa Januari mwaka jana 2016.