Dakta Zarif: Ugaidi si nembo ya dini wala kaumu yoyote ile
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali utendaji wa kindumakuwili wa baadhi ya mataifa kuhusiana na ugaidi.
Dakta Muhammad Javad Zarid ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, ugaidi si nembo ya dini wala kaumu yoyote ile duniani.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria matukio mawili ya kibaguzi na shambulio la kigaidi katika jimbo la Virginia nchini Marekani na Barcelona nchini Uhispania na kusisitiza kwamba, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kweli za kupambana na ugaidi na kutokuweko undumakuwili katika kukabiliana na vitendo vya ugaidi duniani.
Ikumbukwe kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani hakulaani mapema na kutoa radiamali ya haraka dhidi ya shambulio la kibaguzi la mji wa Charlottesville kwenye jimbo la Virginia nchini Marekani kama alivyoharakia kulaani shambulio la kigaidi la Las Ramblas katika mji wa Bacelona nchini Uhspania. Trump alilitaja shambulio la kigaidi la Uhispania kwamba, ni ugaidi wa Kiislamu, hatua ambayo ni undumakuwili wa wazi kuhusu ugaidi.

Itakumbukwa kuwa, katika maandamano ya kupinga ubaguzi yaliyojiri siku ya Jumamosi iliyopita katika mji wa Charlottesville kwenye jimbo la Virginia, kijana mmoja wa kundi linalotetea ubaguzi aliushambulia kwa gari mkusanyiko wa watu waliokuwa wanaandamana kupinga vitendo hivyo na kuua mwanamke mmoja na kujeruhi watu wengine 19.
Aidha watu 13 wameuawa na wengine 100 kujeruhiwa katika shambulizi la juzi Alkhamisi katika eneo la kitalii la Las Ramblas katikati ya jiji la Barcelona, nchini Uhispania. Masaa machache baadaye kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuwa ndilo lililofanya shambulizi hilo.