Rouhani: Iran inatumia nguvu zake kwa ajili ya kujihami
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i33813-rouhani_iran_inatumia_nguvu_zake_kwa_ajili_ya_kujihami
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran ni nchi kubwa na yenye nguvu na uwezo mkubwa na kwamba inatumia uwezo huo kwa ajili ya kujihami.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2017 10:56 UTC
  • Rouhani: Iran inatumia nguvu zake kwa ajili ya kujihami

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran ni nchi kubwa na yenye nguvu na uwezo mkubwa na kwamba inatumia uwezo huo kwa ajili ya kujihami.

Dakta Rouhani ambaye leo alikuwa akihutubia Baraza la Mawaziri amesema Iran ina nyenzo nyingi lakini katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita haijawahi kutumia nguvu na uwezo huo dhidi ya nchi yoyote na daima inatumia nguvu hizo kwa ajili ya kujilinda. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria sikukuu ijayo ya Idil Adh'ha na kusema: Ujumbe mkubwa wa sikukuu hiyo ni kukomesha umwagaji damu katika eneo la Mashariki ya Kati, kurejesha amani na utulivu na kuimarisha upendo wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa, viongozi wa nchi za Kiislamu wanapaswa kujifunga kutokana na siku na sikukuu hizi za Kiislamu ili amani na utulivu virejee katika nchi za eneo hili.

Vilevile amezungumzia tukio la kuuliwa shahidi rais wa zamani wa Iran, Muhammad Ali Rajai na waziri wake mkuu, Muhammad Jawad Bahonar katika shambulizi la kigaidi la kundi la MKO na kusema kuwa, maadui wamefanya kila wawezalo dhidi ya taifa la Iran lakini wananchi wamedumisha njia yao kwa nguvu kubwa zaidi, werevu zaidi na irada na azma kubwa zaidi. 

Muhammad Jawad Bahora na Muhammad Ali Rajai (kulia)

Katika siku kama ya leo ya tarehe 8 Shahrivar (30 mwezi Agosti 1981) kundi la MKO lililipua kwa bomu ofisi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran na kumuua shahidi Rais Muhammad Ali Rajai, Waziri Mkuu wa wakati huo Muhammad Jawad Bahonar na maafisa wengine kadhaa wa serikali.