Rais Rouhani: Iran imekusudia kuimarisha uhusiano wa pande zote na Afrika Kusini
Rais Hassan Rouhani amesema Iran imekusudia kuimarisha uhusiano wa pande zote na nchi za Kiafrika hususan Afrika Kusini.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika mazungumzo na Bi Baleka Mbete, Spika wa Bunge la Afrika Kusini aliyeko safarini hapa nchini.
Akiashiria uungaji mkono wa wananchi wa Iran kwa mapambano ya wananchi wa Afrika Kusini chini ya uongozi wa Nelson Mandela dhidi ya ubaguzi wa rangi, Rais Rouhani amesema: Tehran inakaribisha kuimarisha zaidi ushirikiano na Pretoria katika sekta ya uchumi ikiwemo madini na nishati na iko tayari kutoa ushirikiano na huduma za kiufundi na kiuhandisi kwa Afrika Kusini.
Dakta Rouhani amesema mabunge ya Iran na Afrika Kusini yana nafasi muhimu sana katika kustawishwa na kuimarishwa ushirikiano wa pamoja na akasisitizia udharura wa kustawishwa ushirikiano huo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia misimamo ya pamoja ya Iran na Afrika Kusini katika masuala mengi ya kimataifa na kieneo na kueleza kwamba: Kwa kushirikiana kwa pamoja katika jumuiya za kimataifa, nchi hizi mbili zinaweza kutoa mchango wenye thamani kwa ajili ya kuleta amani na uthabiti duniani na kukidhi manufaa na maslahi ya nchi zinazoendelea.
Akizungumza katika mkutano wake huo na Rais Rouhani, Spika wa Bunge la Afrika Kusini ametilia mkazo azma thabiti ya nchi yake ya kustawisha na kuimarisha zaidi uhusiano wake na Iran katika nyanja zote na kueleza kwamba: Iran na Afrika Kusini inapasa ziimarishe zaidi mashirikiano yao ya pamoja katika duru na jumuiya za kimataifa kwa lengo la kuimarisha amani na urafiki katika uga wa kimataifa.
Bi Baleka Mbete ambaye aliwasili hapa mjini Tehran hapo jana huku akiongoza ujumbe wa Bunge la Afrika Kusini kwa madhumuni ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Iran, kabla ya mazungumzo yake na Rais Rouhani, alikutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Ali Larijani.../