Rais Rouhani: Mafanikio ya mapatano ya nyuklia ya Iran hayawezi batilishwa
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesistiza kuwa, manufaa ya mapatano ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA hayawezi batilishwa na yeyote duniani hata rais wa Marekani.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo Jumamosi katika Chuo Kikuu cha Tehran katika sherehe za kuanza mwaka mpya wa masomo ya vyuo vikuu na taasisi za juu za elimu nchini Iran. Rais Rouhani ameongeza kuwa, yeyote atakayekiuka ahadi na mapatano atatia dosari katika itibari yake katika hali ambayo Iran imechagua mkondo sahihi na inafungamana na ahadi zake.
Rais Rouhani amesema mapatano ya JCPOA ni ushindi wa kimaadili wa Iran katika uga wa kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani. Ameongeza kuwa: "Kabla ya JCPOA, baadhi walikuwa wakidai kuwa shughuli za nyuklia za Iran ni kinyume cha sheria na kwamba Iran haina haki ya kurutubisha madini ya urani lakini hivi sasa wametambua haki za Iran katika uga wa nyuklia.
Rais wa Iran amewatahadharisha maadui kwa kusema: "Iwapo nchi yoyote itaihujumu Iran, ifahamu kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine itaibuka mshindi."
Itakumbukwa kuwa Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilifikia mapatano kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran. Mapatano hayo ambayo ni maarufu kama JCPOA yalifikiwa Julai 2015 na kuanza kutekelezwa Januari 16 mwaka jana. Kwa mujibu wa mapatano hayo, Iran ilitakiwa kupunguza baadhi ya shughuli zake za nyuklia huku nchi za Magharibi zikitakiwa ziiondolee Iran vikwazo. Lakini pamoja na hayo Marekani inakaidi mapatano hayo huku Rais Donald Trump wa nchi hiyo akitishia kuiondoa nchi yake katika JCPOA.