Iran kamwe haitaruhusu vituo vyake vya kijeshi kukaguliwa
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa kamwe haitaruhusu vituo vyake vya kijeshi vikaguliwe huku mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Atomiki IAEA akiwasili mjini Tehran.
Hayo yamesemwa na Behrouz Kamalvandi msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran ambaye ameongeza kuwa kadhia ya kukaguliwa vituo vya kijeshi vya Iran haipo katika mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 baina ya Iran na madola makuu sita duniani. Amesema kile ambacho IAEA inaweza kuomba ni kukagua vituo vya nyuklia vya Iran.
Kamalvandi amesisitiza kuwa, Iran inatekeleza shughuli zake za nyuklia katika vituo ambavyo vinafahamika na IAEA na kwa msingi huo hakuna haja ya kukagua maeneo mengine yawe ni ya kijeshi au yasiyo ya kijeshi.
Msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran ametoa wito kwa IAEA kutekeleza majukumu yake kwa njia huru na kwa utaalamu pasina kulegeza msimamo mbele ya mashinikizo.
Tarehe 14 Julai mwaka 2015 Iran na China, Russia, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani zilifikia makubaliano ya nyuklia kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran baada ya mazungumzo magumu na ya muda mrefu. Makubaliano hayo ambayo yanajulikana kwa kifupi kwa jina la JCPOA, tarehe 20 Julai mwaka huo huo wa 2015 yalipasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuwa hati ya kimataifa.
Safari ya Amano nchini Iran inakuja huku kukiwa na mgogoro baina ya Iran na Marekani baada ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kutoa taarifa hivi karibuni na kudai kuwa eti Iran haifungamani na JCPOA. Nchi zingine za 5+1 zimekosoa vikali msimamo huo wa Marekani na kusisitiza kuwa Iran inatekeleza ahadi zake kwa mujibu wa mapatano.