Rouhani: Watawala wa Saudia wanajua vyema nguvu za Iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel daima zinayatakia mabaya mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati na zinatumia visingizio vya aina mbalimbali kwa ajili ya kuwepo katika eneo hilo na kupora mafuta na utajiri wake.
Dakta Hassan Rouhani amesema madola makubwa ya Magharibi yanafanya mikakati ya kuzusha migawanyiko na hitilafu baina ya mataifa na nchi mbalimbali na kusisitiza kuwa ana matumaini watawala wa nchi za Mashariki ya Kati wataelewa uhakika huo na kukhitari njia ya umoja na mshikamano baina ya mataifa yao.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema serikali ya Marekani ina utaalamu makhsusi wa kupora utajiri wa nchi mbalimbali hususan Saudi Arabia na inadumisha vita na machafuko eneo la Mashariki ya Kati kupitia njia ya mauzo ya silaha.
Ameashiria uadui wa Saudi Arabia dhidi ya mataifa ya eneo hilo hususan mataifa ya nchi za Iraq, Syria na Yemen na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiyatakii mataifa mengine isipokuwa kheri, ufanisi, amani na usalama kwa nchi zote ikiwemo Saudi Arabia yenyewe.
Rais Rouhani amewaambia watawala wa Saudi Arabia kwamba: Mnajua vizuri nguvu na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran na wale wenye nguvu zaidi kuliko nyinyi wameshindwa kufanya chochote dhidi ya taifa la Iran".
Ametilia mkazo udharura wa kusitishwa mashambulizi na mabomu dhidi ya nchi za eneo hili na kusema: Tuhuma kwamba Iran inaingia masuala ya ndani ya nchi nyingine zinatolewa katika kipindi ambacho Iran inazisaidia nchi za Iraq na Syria kupambana na ugaidi na mapambano hayo yamebatilisha njama za makundi ya kigaidi kama Daesh.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaambia viongozi wa Saudi Arabia kwamba: "Kama mnadhani kuwa Iran si rafiki yenu na kwamba Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ndio marafiki wenu basi mnafanya makosa makubwa ya kimahesabu na kistratijia".