Rouhani: Maadui wanataka kuzusha mgogoro mpya Mashariki ya Kati
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, baada ya njama zao kushindwa sasa maadui wanapanga mikakati ya kuzusha njama mpya katika eneo la Mashariki ya Kati.
Rais Rouhani ameashiria mafanikio ya watu wa eneo hilo katika vita dhidi ya magaidi na kusema kuwa: Hii leo watu wa Iraq, Syria na Lebanon wakisaidiana na majeshi ya nchi hizo na masaada wa nchi rafiki hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wamefanikiwa kuondokana na matatizo hayo, na kwamba kadhia ya ugaidi inaelekea kumalizwa kabisa. Ameongeza kuwa, njama za maadui za kutaka kuzigawa nchi za Mashariki ya Kati na kuvuruga mipaka ya kijiografia ya eneo hili pia zimefeli na mafanikio hayo yameikasiri sana Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na vibaraka wao.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kwa miaka kadhaa sasa ambapo wananchi maskini wa Yemen wanashambuliwa kwa mabomu na kusumbuliwa na kipindupindu na njaa huku wakizingirwa kutoka angani, nchi kavu na baharini. Rais Rouhani amesisitiza kuwa jambo hilo haliwezi kustahamiliwa.
Dakta Rouhani amesema kuwa hali ya sasa ya Mashariki ya Kati inaonesha kuwa, maadui wanapanga njama mpya katika eneo hilo na kwamba watu wa nchi za Mashariki ya Kati wanapaswa kuwa macho na makini na viongozi wanalazimika kuchukua hatua zinazostahili.