Zarif: Iran iko Syria kwa "ombi rasmi" la serikali ya Damascus
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwepo Iran nchini Syria kumetokana na ombi rasmi la serikali ya nchi hiyo.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa mashambulio makali yaliyofanywa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kubadilisha mlingano wa nguvu za kijeshi katika Mashariki ya Kati kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Kufuatia hatua hiyo Syria iliziomba Iran na Russia ziisaidie katika vita vya kupambana na magaidi.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mkutano wa kimataifa wa mazungumzo ya Mediterania unaofanyika katika mji mkuu wa Italia, Rome.
Katika mkutano huo, Zarif aidha ameashiria uungaji mkono wa baadhi ya nchi za eneo kwa makundi ya kigaidi yakiwemo ya Daesh, Jabhatu-Nusra na Taliban na kueleza kwamba nchi hizo zingali zinaendelea kuchukua hatua hizo ghalati.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, baadhi ya nchi zinadhani kwamba badala ya kujenga maelewano na majirani zao zitaweza kuinunua amani na usalama kwa kununua silaha na kubainisha kwamba: sote tunapaswa kushirikiana pamoja ili kuigeuza Mashariki ya Kati mahali salama pa kuishi.
Zarif aidha ameongeza kwamba Saudi Arabia imeyakataa machaguo yote kwa ajili ya usitishaji vita na kufikiwa suluhu katika nchi za Syria na Yemen.../