Maandamano ya wananchi wa Iran kulaani fujo na ghasia za hivi karibuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i38559-maandamano_ya_wananchi_wa_iran_kulaani_fujo_na_ghasia_za_hivi_karibuni
Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya Sala ya Ijumaa wameshiriki kwenye maandamano makubwa katika maeneo mbali mbali nchini, ukiwemo mji mkuu Tehran, kulaani fujo na ghasia zilizozushwa hivi karibuni huku wakitaka wahusika wa fitina hizo wachukuliwe hatua kali kisheria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 05, 2018 11:14 UTC
  • Maandamano ya wananchi wa Iran kulaani fujo na ghasia za hivi karibuni

Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya Sala ya Ijumaa wameshiriki kwenye maandamano makubwa katika maeneo mbali mbali nchini, ukiwemo mji mkuu Tehran, kulaani fujo na ghasia zilizozushwa hivi karibuni huku wakitaka wahusika wa fitina hizo wachukuliwe hatua kali kisheria.

Katika siku kadhaa zilizopita baadhi ya watu kwenye miji kadhaa nchini Iran walifanya mikusanyiko na maandamano kulalamikia masuala mbalimbali ikiwemo kutojulikana hatima ya watu waliopata hasara na kupoteza fedha zao katika taasisi za fedha, ughali wa baadhi ya bidhaa na udhaifu wa serikali katika usimamizi wa mambo ya nchi. Hata hivyo baadhi ya maandamano hayo yalitumiwa vibaya na watu wenye nia mbaya na wahuni wanaoungwa mkono na baadhi ya nchi za Magharibi, za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel kuzusha fujo na machafuko.

Kufuatia fitina hiyo, tokea siku ya Jumatano, wananchi wa Iran katika miji mbalimbali wamekuwa wakishiriki katika maandamano makubwa ya kulaani njama hizo za maadui na wahuni waliotumia fursa hiyo kuharibu mali za uma.

Wairani katika maandamano ya kuipinga Marekani na waitifaki wake na kuunga mkono mfumo wa Kiislamu 

Kwa mujibu wa mwandishi wa Radio Tehran, siku ya Ijumaa pia, wananchi kote katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamejitokeza kwa wingi wakiwa wamebeba mabango na kutoa nara za kuunga mkono mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha waandamanaji wamesisitiza kuhusu ulazima wa kukabiliana na fitina zilizozushwa na Marekani na waitifaki wake. Washiriki wa maandamano hayo wametoa nara za "Mauti kwa Marekani" na "Mauti kwa Israel" huku wakiteketeza bedera za tawala hizo mbili. Waandamanaji hao pia wametoa nara za "Mauti kwa Aal Saud" na kuulani utawala wa Saudia kwa kushirikiana na Wamarekani na Wazayuini kuchochea fitina na ghasia nchini Iran.

Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesisitizia ulazima wa taifa kutumia busara na hekima katika kukabiliana na fitina huku wakisisitiza kuwa wako tayari kujitolea muhanga kuilinda nchi yao.