Qassemi: Iran imefanikiwa kuzima mapema njama za serikali ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i38691-qassemi_iran_imefanikiwa_kuzima_mapema_njama_za_serikali_ya_marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, hamu kubwa ya wananchi wa Iran ya kushiriki vilivyo katika kujiamulia wenyewe mambo yao, daima imekuwa ikizima mapema njama za kila namna za Marekani.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Jan 08, 2018 13:03 UTC
  • Qassemi: Iran imefanikiwa kuzima mapema njama za serikali ya Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, hamu kubwa ya wananchi wa Iran ya kushiriki vilivyo katika kujiamulia wenyewe mambo yao, daima imekuwa ikizima mapema njama za kila namna za Marekani.

Bahram Qassemi amesema hayo leo katika mazungumzo yake ya kila wiki na waandishi wa habari wa ndani na nje na huku akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wa Radio Tehran kuhusiana na kikao cha masuala ya usalama kilichofanyika leo hapa Tehran na njama za Marekani za kutaka kuutia usalama wa Iran katika matatizo amesema: Siasa za chuki na uadui za Marekani ambayo zinajaribu kuiweka Iran katika changamoto za kila namna daima zimekuwa zikifeli.

Bahram Qassemi akijiandaa kuzungumza na waandishi wa habari

 

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekumbushia namna siasa za mambo ya nje za Marekani zilivyofeli vibaya katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kuongeza kuwa: Rais wa Marekani, Donald Trump ndiye mchochezi mkuu wa mgogoro katika eneo hili.

Vile vile amezungumzia kikao cha dharura kilichoitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mashinikizo makubwa ya Marekani ili kujadili machafuko yaliyotokea hivi karibuni nchini Iran na namna wanachama wa baraza hilo walivyopuuza madai hayo ya Marekani na kusisitiza kuwa masuala hayo yalikuwa yanahusu ndani ya Iran na hayahusiani kabisa na Umoja wa Mataifa. Amesema: Majibu ya hapana aliyopigwa nayo Trump ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni muendelezo wa kufeli siasa za Marekani katika eneo hili na duniani kiujumla.

Amma kuhusiana na meli ya mafuta ya Iran iliyoungua katika fukwe za China wakati ilipokuwa inaelekea Korea Kusini amesema: Licha ya kutumwa helikopta na meli za kutoa misaada lakini bado hali si salama.