Iran yaunga mkono juhudi za kutatua matatizo ya Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39617-iran_yaunga_mkono_juhudi_za_kutatua_matatizo_ya_iraq
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonana na mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iraq na kubadilishana naye mawazo kuhusu masuala na matukio mbalimbali ya nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 29, 2018 01:07 UTC
  • Iran yaunga mkono juhudi za kutatua matatizo ya Iraq

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonana na mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iraq na kubadilishana naye mawazo kuhusu masuala na matukio mbalimbali ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Mazungumzo ya jana Jumapili ya hapa mjini Tehran, kati ya Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Yan Kubish, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iraq, yalijikita katika matukio ya hivi karibuni ya nchi hiyo na umuhimu wa kulindwa amani na utulivu nchini Iraq.

Pande hizo mbili zimehimiza pia wajibu wa kushirikiana na kuwamaliza mabaki ya magaidi wa Daesh (ISIS) na pia kufanyika uchaguzi wa bunge kwa haki na amani huko Iraq kama ambavyo Iran na Umoja wa Mataifa zimesisitizia pia udharura wa kushiriki makundi na vyama vyote vya kisiasa katika uchaguzi huo.

Magaidi wa Daesh (ISIS) walifanya jinai kubwa walipoivamia Iraq mwaka 2014. Hapa wakiwapiga risasi na kuwaua kwa umati watu waliowateka nyara

 

Mjumbe huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alionana pia na Dk Ali Akbar Velayati, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa.

Baada ya mazungumzo yao, Yan Kubish, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iraq aliwaambia waandishi wa habari kuwa umoja huo unawaunga mkono kikamilifu wananchi na kulindwa umoja wa ardhi nzima ya Iraq. Vile vile ameelezea matumaini yake kwamba serikali ya Baghdad itatimiza wajibu wake katika kudumisha amani na utulivu ndani ya Iraq na kwenye eneo hili zima.