Iran: Jibu letu kwa Israel litaisambaratisha Tel Aviv kikamilifu
Katibu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu ya Iran, ameonya kuwa, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni utageuzwa majivu Tehran ikilazimika kujibu mapigo iwapo Benjamin Netanyahu atatekeleza vitisho vyake alivyovitoa hivi karibuni dhidi ya taifa hili.
Katika mahojiano na kanali ya habari ya al-Manar, Mohsen Rezaee amesema, "Kuhusu kauli isiyo na hekima ya Netanyahu, niseme kuwa iwapo watajaribu kuchukua hatua yoyote ya kipuzi dhidi ya Iran, tutaisambaratisha Tel Aviv kikamilifu na hatutaoa fursa yoyote kwa Netanyahu kutoroka."
Akihutubia mkutano wa usalama wa Munich nchini Ujerumani Jumapili iliyopita, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel huku akiwa amebeba kile alichokitaja kama pande la mabaki ya ndege isiyo na rubani ya Iran aliyodai eti imetunguliwa na jeshi la Israel zaidi ya wiki moja iliyopita, alidai kuwa Tel Aviv ina uwezo wa kutoa jibu la moja kwa moja dhidi ya Iran.
Katibu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, Marekani na Israel hazina ufahamu wowote kuhusu Iran, wala hawajadiriki uwezo wa muqawama, na ndiposa wanaendelea kushindwa vibaya kila siku.
Akijibu matamshi ya Netanyahu hivi karibuni, Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Brigedia Jenerali Salami alisema kuwa, hatua ya maonyesho na mchezo wa kuigiza ya viongozi wa Marekani na utawala haramu wa Israel inaonyesha kuwa, nafasi na daraja yao imeshuka na wanakabiliwa na mazingira magumu katika kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Kwa upande wake, Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamun ya Iran ameyataja matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu katika kikao cha Munich kama mchezo wa kuigiza wa katuni, ambayo hayana hata thamani ya kujibiwa.