Rais Rouhani wa Iran ampongeza Ramaphosa, Rais mpya wa Afrika Kusini
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtumia salamu za pongezi Cyril Ramaphosa kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Afrika Kusini.
Katika ujumbe wake Jumapili, Rais Rouhani ameelezea matumaini yake kuwa, uhusiano wa Iran na Afrika Kusini utazidi kuimarika katika viwango vya pande mbili na kimataifa.
Aidha Rais Rouhani amemtakia mafanikio Rais Ramaphosa pamoja na watu wa Afrika Kusini.
Itakumbukwa kuwa mnamo Februari 15, Bunge la Afrika Kusini lilimchagua Cyril Ramaphosa ambaye ni Mwenyekiti wa chama tawala cha ANC kuwa rais mpya wa nchi hiyo.
Hatua hiyo ilichukuliwa na Bunge la Afrika Kusini baada ya kujiuzulu rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma.
Bunge la Afrika Kusini lenye wabunge 400 ambalo linadhibitiwa na chama cha ANC, lilimchagua Ramaphosa kukamilisha kipindi cha uongozi wa Zuma kitakachomalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka kesho wa 2019.
Jacob Zuma mwenye umri wa miaka 75 alilazimika kujiuzu kutokana na mashinikizo ya chama chake cha ANC kilichokuwa kimempa masaa 48 kung'atuka madarakani.