Mar 22, 2018 06:57 UTC
  • Matamshi ya Kiongozi Muadhamu kuhusiana na matukio mbalimbali ya kieneo

Jumatano ya jana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alikutana na idadi kubwa ya wafanya ziara na wakazi wanaoishi jirani na Haramu Tukufu ya Imam Ridha (as) mjini Mash'had kwa mnasaba wa sikukuu ya Nairuzi, ambapo alitoa ufafanuzi jumla kuhusiana na matukio mbalimbali ya eneo la Mashariki ya Kati na masuala ya dharura ya kiuchumi pamoja na mambo mengine muhimu.

Akiashiria juu ya uimara na nishati ya Mapinduzi ya Kiislamu katika kipindi cha uhai wake wa miaka 40 na kadhalika kusambaratishwa njama chafu za Marekani katika eneo hili, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, katika mwaka uliopita wa 1396 Hijiria Shamsia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliweza kupeperusha bendera ya izza na uwezo wa taifa la Iran katika eneo, huku ikiwa pia na nafasi muhimu katika kuwashinda magaidi wakufurishaji na kuimarisha usalama. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kusisitiza kwamba, hatua hizo za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimesambaratisha njama chafu za Marekani katika eneo ameongeza kuwa, Wamarekani kwa kuanzisha makundi ya 'shari, ya kidhalimu na yanayotenda jinai' kama vile Daesh (ISIS) na mengine mfano wa hilo, walikusudia kuyashughulisha mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati na vita vya ndani na wakati huo huo kuyasahaulisha na hatari ya utawala ghasibu wa Kizayuni.

Mfalme Salman wa Saudia akimvisha mkufu wa dhahabu Trump, ambao wote wapanga njama dhidi ya Iran

Aidha akibainisha ramani ya njama hizo na kadhalika madai bandia ya Wamarekani kwamba wamehusika katika kulitokomeza kundi la Daesh, Kiongozi Muadhamu amesisitiza kwa kusema: "Madai hayo ya Marekani ni ya uongo, kwani siasa za Marekani zimesimama juu ya msingi wa kulilinda kundi hilo la Daesh (ISIS) na mfano wake, madamu makundi hayo yapo chini ya himaya ya Wamarekani." Marekani haijafanikiwa katika njama hizo na ndio maana ikawa inashirikiana na baadhi ya washirika wake wa Ulaya kuibua tuhuma kila uchao dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Umuhimu wa hotuba ya Kiongozi Muadhamu unashuhudiwa hasa kwa kuzingatia malengo ya Marekani katika kuibua ghasia na machafuko ndani ya eneo la Mashariki ya Kati, ambapo dhumuni la njama hizo ni kutoa pigo kwa taifa la Iran ya Kiislamu. Ukweli ni kwamba Marekani, haina sifa yoyote ya kuweza kulisambaratisha kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) na zaidi ya hayo ni kwamba Washington haina uwezo wa kudhamini usalama wa eneo hili.

Pande tatu mashuhuri zinazopanga njama dhidi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mfano wa ukweli huo kuwa ni uwepo wa miaka 14 wa Marekani nchini Afghanistan, ambao si tu kwamba uwepo huo haujakuwa na faida yoyote ya maana kwa wananchi wa taifa hilo, bali ni kwamba hali ya usalama na amani ya nchi hiyo imezidi kuwa mbaya kila siku. Ukweli ni kwamba migogoro, machafuko na vita ambavyo vimezikumba baadhi ya nchi za eneo la magharibi mwa Asia, vimeratibiwa kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja na Marekani yenyewe. Kuhusiana na suala hilo, Noam Chomsky, mwananadharia mashuhuri wa nchini Marekani amebainisha malengo ya uingiliaji wa Marekani katika nchi nyingi kwa kusema: "Marekani ndio msababishi wa vita na mizozo ya kimataifa na ni muhusika pia wa mapinduzi ya kijeshi dhidi ya tawala mbalimbali. Mfano wa hilo ni mapinduzi ya tarehe 28 Mordad, sawa na Agosti 1953 dhidi ya serikali halali ya Iran." Mwisho wa kunukuu.

Noam Chomsky, mwananadharia mashuhuri wa nchini Marekani

Hata hivyo taifa la Iran katika kipindi chote hiki limeonyesha azma ya hali ya juu katika kukabiliana na njama za Marekani na katika uwanja huo, limekuwa likifikia melengo yake. Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kuimarisha usalama ndani ya eneo la Mashariki ya Kati na baada ya hayo pia itaendelea na mkondo huo huo. Aidha katika sehemu nyingine ya hotuba yake ya jana, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, aliashiria masuala muhimu kwa ajili ya kulifikisha taifa la Iran kwenye kilele cha uchumi wenye nguvu na ulio imara.

Bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu, kwa kuwa na nguvukazi ya wataalamu waliohitimu katika vyuo vikuu, vyanzo muhimu vya nishati kama vile mafuta na gesi na kadhalika uwezo mzuri wa uzalishaji, Iran ya Kiislamu  ina nafasi yenye nguvu ambayo kwa kutegemea vyanzo hivyo, itaweza kufikia maendeleo ya haraka katika mwaka mpya huu wa 1397 Hijiria Shamsia na hivyo kuifanya nchi hii ifikie malengo yake tarajiwa. Kwa msingi huo, nukta muhimu ambazo zimeashiriwa na Kiongozi Muadhamu katika hotuba ya jana katika Haram ya Imamu Ridha (as) mjini Mash'had, zinaweza kuwa na nafasi chanya katika kubainisha ramani ya njia ya mustakbali wa taifa na pia kuwa chanzo cha kuwa macho mkabala wa malengo ya shari ya Marekani ndani ya eneo la Mashariki ya Kati.

Tags