Iran yaomboleza kifo cha mwanamapambano mwenza wa Mandela, Winnie
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kufuatia kuaga dunia Bi. Winnie Mandela, mwanamapambano mwenza wa hayati Shujaa Nelson Mandela kiongozi wa harakati ya kupambana na mfumo wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
Katika salamu zake za rambi rambi kwa serikali na taifa la Afrika Kusini, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif amesema: "Kuaga dunia Bi. Winnie Mandela si tu kuwa ni pigo na msiba kwa watu wa Afrika Kusini na bara Afrika, bali pia kwa watu wote duniani ambao walivutiwa na kupata ilhamu katika fikra za Mandela katika mapambano ya kupigania uhuru na kukabiliana na ubaguzi wa rangi."
Zairf ameashiria historia ndefu ya mapambano ya Winnie Mandela hasa kipindi cha miongo minne ya mapambano makali dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi na makaburu chini ya uongozi wa Shujaa Mandela, na kusema katika kipindi hiki cha majonzi anashikamana na wale wote wanaopenda na kuvutiwa na fikra za Nelson Mandela.

Winnie Mandela, mwanamapambano na mke wa zamani wa Shujaa Mandela alifariki dunia Jumatatu, Aprili 2, 2018 akiwa na umri wa miaka 81.
Winnie Mandela alikuwa mmoja wa wanaharakati wa mstari wa mbele wa kupambana na utawala wa kibaguzi wa makaburu wa Afrika Kusini.
Msemaji wa familia hiyo, Victor Dlamini amesema katika taarifa yake kwamba Winnie Mandela amefariki dunia katika hospitali moja mjini Johannesburg baada ya kuugua kwa muda mrefu.