Jeshi la Iran lasema haliwezi kupigishwa magoti na maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43534-jeshi_la_iran_lasema_haliwezi_kupigishwa_magoti_na_maadui
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katu Iran haiwezi kupigishwa magoti na kukubali matakwa ya maadui wa taifa hili wakiongozwa na Marekani na waitifaki wake.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 23, 2018 03:31 UTC
  • Jeshi la Iran lasema haliwezi kupigishwa magoti na maadui

Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katu Iran haiwezi kupigishwa magoti na kukubali matakwa ya maadui wa taifa hili wakiongozwa na Marekani na waitifaki wake.

Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri ameyasema hayo leo Jumatatu katika ufunguzi wa Duru ya 6 ya Warsha ya Vikosi vya Majini vya Bahari Hindi (IONS) hapa mjini Tehran.

Jumbe 35 za ngazi za juu za Vikosi vya Baharini kutoka sehemu mbali mbali duniani zinashiriki mkutano huu, ambapo Iran imekabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo kwa muhula mmoja wa miaka miwili.

Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, nchi za kibeberu zimekataa kukubali ukweli wa mambo kwamba, mfumo waliokuwa wakiupigia debe wa 'World Order' umeperaganyika na kwamba kwa sasa kuna ujio wa kasi wa mataifa yenye nguvu kubwa kutoka Mashariki na Magharibi.

Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri

Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri amesisitiza kuwa, "Hatua ya Marekani ya kuliunga mkono kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) imesababisha kuvurugika kwa usalama na uthabiti, mbali na maafa ya watu na miundomsingi ya nchi za Asia Magharibi."

Amesema mfano hai wa mataifa ya kibeberu kuchukua hatua zilizo kinyume cha sheria ni kitendo cha hivi karibuni cha Marekani, Ufaransa na Uingereza kuvurumisha makombora dhidi ya Syria, katika hali ambayo nchi hizo za Magharibi zimekuwa zikirundika silaha katika nchi za Mashariki ya Kati kama vile Saudi Arabia, ili kulitumbukiza eneo hili katika vita.