Iran: Hakuna kilichosimama nchini hapa baada ya Trump kujiondoa JCPOA
Behrouz Kamalvandi, Msemaji wa Shirika la Nyuklia la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuashiria sisitizo la Ulaya la kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na Iran amesema kuwa, utendajikazi wa Ulaya hususan juu ya mapatano ya nyuklia ya Iran JCPOA unaendelea vizuri na kwamba hakuna kitu kilichosimama kwa sababu ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo.
Kamalvandi ameyasema hayo kando ya kikao cha ujumbe wa Ulaya unaoongozwa na kamisheni ya nyuklia ya Umoja huo pamoja na ujumbe wa kamati ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Akijibu swali kuhusiana na hatua zilizochukuliwa na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran katika radiamali yake kufuatia hatua ya Marekani ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia amesema: "Ikiwa tutaweza kufikia maelewano na EU ya kuendeleza na mapatano hayo bila ya Marekani, basi tunaweza kuendeleza makubaliano ya JCPOA kwa ushirikiano wetu wenyewe na pande nyingine za mapatano thayo."
Aidha Msemaji wa Shirika la Nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria ushirikiano wa pande za Ulaya kuhusiana na kadhia hiyo na kusema, hivi sasa Ulaya imeonyesha kwa uchache irada ya kulinda mapatano hayo kama ambavyo pia imeonyesha azma yake ya kuendeleza ushirikiano na Iran. Hata hivyo amesisitiza kwamba irada hiyo bado haitoshi kwa ajili ya kuifanya Tehran iendelee kubakia katika makubaliano hayo. Sambamba na kubainisha kwamba Marekani imejikuta katika mazingira mabaya kuhusu itibari yake kimataifa amesema kuwa, mazungumzo ya jana ya ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya yalikuwa chanya na kwamba Iran bado inaendeleza mazungumzo na pande za China, Russia na Umoja wa Ulaya kuhusu kadhia hiyo.
Akijibu swali kuhusu hatua itakayochukuliwa na Iran iwapo mazungumzo yanayoendelea sasa na Ulaya hayatozaa matunda, amesema kuwa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran limejiandaa kwa ajili ya mazingira yote, kukiwemo kurundi katika hali yake ya nyuma au zaidi ya hapo katika uga wa kurutubisha urani. Amesisitiza kwamba hatua ya Rais Donald Trump ya kuiondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia haijakuwa na athari yoyote nchini Iran na kwamba mambo yanaendelea kama kawaida.