Iran inaunga mkono Palestina katika kutekeleza wajibu wa kidini na kiitikadi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45312-iran_inaunga_mkono_palestina_katika_kutekeleza_wajibu_wa_kidini_na_kiitikadi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono harakati za ukombozi wa Palestina kwa msingi wa kiitikadi na kutekeleza wajibu wa kidini.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Jun 02, 2018 13:19 UTC
  • Iran inaunga mkono Palestina katika kutekeleza wajibu wa kidini na kiitikadi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono harakati za ukombozi wa Palestina kwa msingi wa kiitikadi na kutekeleza wajibu wa kidini.

Kauli hiyo imetolewa na Admeri Ali Shamkhani Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran katika mahojiano na gazeti la kila siku la Sharq la hapa Iran. Ameongeza kuwa: "Iran imefanya mazungumzo na nchi nyingi za Kiislamu kuhusu  hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kusitisha masaibu ya Wapalestina." Amesema Iran pia inatumia mbinu mbali mbali kama vile ya vyombo vya habari  ili kuakisi kimataifa dhulma wanazotendewa Wapalestina kwa lengo la kuishinikiza Marekani na kuutenga zaidi utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran pia ameashiria kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds Tukufu (Jerusalem) na kusema: "Uamuzi huo usiokuwa wa busara wa Marekani umepelekea ulimwengu wa Kiislamu kuungana zaidi na pia kuwepo mshikamano zaidi miongoni mwa makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina."

Shamkani ameendelea kusema kuwa, utawala wa Kizayuni ni adui sugu wa Iran na kwamba utawala huo umetekeleza jinai nyingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameongeza kuwa kuibuka makundi ya magaidi wakufurishaji katika eneo, na kuangamizwa kiwango kikubwa cha miundo msingi muhimu ya kiuchumi na kijeshi ya nchi za Kiislamu ni mambo ambayo yalikuwa yameuandalia utawala wa Israel miaka kadhaa ya usalama lakini hatua ya Iran kuyaangamiza makundi hayo ya magaidi wakufurishaji huko Syria na Iraq kumepelekea Israel kupoteza hali hiyo ya kujihisi kuwa salama.

Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Tanzania

Shamkhani amesisitiza kuwa, kuangamizwa magaidi katika eneo kumepelekea kadhia ya Palestina kwa mara nyingine kuwa kadhia nambari moja katika ulimwengu wa Kiislamu. Amesema sera za Iran katika eneo zimejengeka katika msingi wa kupinga chochote kinachovuruga usalama wa nchi za eneo, kutetea wanaodhulumiwa na kupambana na ugaidi.

Ikumbukwe kuwa kufuatia ubunifu wa Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ilitangazwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds. Katika siku hii Waislamu na wapenda haki kote duniani hujumuika ili kubainisha kuchukizwa kwao na sera za kibaguzi za utawala wa Kizayuni wa Israel huku wakitangaza kuunga mkono malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.

Mwaka huu tarehe 8 Juni sawa na 23 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani itakuwa Siku ya Kimataifa ya Quds.