Shamkhani: Trump ameifanya US itengwe kisiasa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Kushamiri vitendo vya ukatili vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan ni hatua ya kutapatapa inayochukuliwa baada ya kushindwa mpango na njama ya kuwatumia magaidi wa kitakfiri ili kuzusha mapigano katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Ali Shamkhani amebainisha kuwa kurejea usalama katika nchi za Syria na Iraq ni kengele ya hatari ya kufikia tamati hali ya ushwari kamili wa usalama kwa utawala wa Kizayuni na kubadilika tena kadhia ya Palestina kuwa suala la kwanza kwa Ulimwengu wa Kiislamu.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameongeza kuwa leo makundi ya muqawama na fikra za waliowengi katika Ulimwengu wa Kiislamu zimezidi kubainikiwa na ukweli, kwamba kiu ya wendawazimu ulionao utawala wa Kizayuni ya kutaka kujitanua zaidi na kushadidisha uvamizi haiwezi kupungua kwa kufanya mazungumzo na Marekani na kuridhia matakwa ya utawala huo ghasibu.
Shamkhani amebainisha pia kwamba kususiwa Marekani katika kikao cha karibuni cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni tukio la kudhalilisha kwa nchi hiyo na nadra kushuhudiwa, na akaongeza kwamba, rasimu ya azimio lililopendekezwa na Marekani la kutaka harakati ya Hamas itambuliwe na kulaaniwa kama msababishaji wa matukio yanayojiri katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu lilishindwa kupata hata kura moja ya uungaji mkono.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza kuwa kujitenga washirika wa jadi wa Marekani na nchi hiyo ni ithbati kwamba siasa zisizo na busara za Trump zimeifanya Washington itengwe kisiasa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.../