Kufanyika amali za Lelatul Qadr nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45398-kufanyika_amali_za_lelatul_qadr_nchini_iran
Amali za usiku mtukufu wa kwanza wa Lelatul Qadr zimefanyika katika pembe zote za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo umati mkubwa wa waumini umeshiriki ibada za usiku huu mtukufu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 04, 2018 03:23 UTC
  • Kufanyika amali za Lelatul Qadr nchini Iran

Amali za usiku mtukufu wa kwanza wa Lelatul Qadr zimefanyika katika pembe zote za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo umati mkubwa wa waumini umeshiriki ibada za usiku huu mtukufu.

Jana usiku ambao ni usiku wa kuamkia leo tarehe 19 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, waumini wamekusanyika katika maeneo tofauti ya ibada ikiwemo misikiti, haram, husseinia, na vituo vya utamaduni ili kuhuisha usiku huu mtukufu na wenye thamani kubwa katika kalenda ya Kiislamu. Katika usiku huu ambao vilevile unasadifiana na siku ya kupigwa upanga Imam Ali (as), waumini walishirika pia katika maombolezo ya mtukufu huyo wa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw). Katika mji mtakatifu wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran, ambako amezikwa Imam Ali Ridha (as), Imam wa Nane wa Mashia na amabye ni mjukuuu wa Mtume (saw), waumini kutoka pembe tofauti za Iran na dunia walikusanyika hapo kwa madhumuni ya kutekeleza ibada hiyo muhimu ya kuhuisha usiku wa Leilatul Qadr na wakati huohuo kuomboleza tukio chungu la kupigwa upanga Imam Ali ambaye ni Imam wa kwanza, sahaba na msaidizi mkubwa na wa karibu wa Mtume wa Uislamu (as).

Waumini wakihuisha usiku wa Lelatul Qadr katika haram ya Imam Ridha (as) mjini Mash'had

Amali kama hizo za Leilatul Qadr na pia maombolezo ya Imam Ali (as) yalifanyika katika Haram ya Bibi Fatwimah Masuma (sa) katika mji mtakatifu wa Qum, kusini mwa Tehran na pia katika Haram ya Ahmad bin Musa Shahchiragh (as) huko Shiraz, makao makuu ya Mkoa wa Fars, kusini mwa Iran. Usiku wa Lelatul Qadr katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ni usiku mtukufu na ambao una fadhila nyingi sana kwa kadiri kwamba amali katika usiku huu ni bora kuliko amali za miezi elfu moja na ni usiku ambao Mwenyezi Mungu huwakadiria waja wake masuala yao ya mwaka  mzima.