Iran yaifahamisha IAEA kuhusu kuanza kuzalisha gesi za UF6 na UF4
(last modified Tue, 05 Jun 2018 07:02:58 GMT )
Jun 05, 2018 07:02 UTC
  • Iran yaifahamisha IAEA kuhusu kuanza kuzalisha gesi za UF6 na UF4

Iran imeufahamisha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuwa imeanzisha mchakato wa kuimarisha uwezo unaohitajika wa kuzalisha gesi aina ya UF6 na UF4 na ujenzi wa kiwanda cha kutengenza mashinepewa (centrifuge).

Gesi za UF6 na UF4 hutumika katika mashinepewa wakati wa kurutubisha madini ya urani yanayotumika katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia.

Msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran Behrouz Kamalvandi katika mahojiano na Shirika la Habari la ISNA, ameashiria hotuba ya jana ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Haram ya Imam Khomeini MA na kusema: "Kwa kuzingatia amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa Shirika la Atomiki la Iran linawajibika, katika fremu ya mapatano ya JCPOA, kufuatilia suala la kuimarisha urutubishaji urani hadi kufikia kiwango cha SWU 190,000, shirika hilo linapaswa kuanzisha mchakato huo kwa kasi."

Katika hotuba yake Jumatatu alasiri katika maadhimisho ya mwaka wa 29 tokea alipoaga dunia Imam Khoemini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Kiongozi Muadhamu alitoa amri kwa Shirika la Atomiki la Iran na kusema: "Matayarisho yanayohitajika kwa ajili ya kufikwa kiwango cha SWU 190,000 yaanze kutekelezwa haraka katika fremu ya mapatano ya JCPOA." 

Mashinepewa katika taasisi ya nyuklia ya Natanz nchini Iran

Msemaji wa Shirika la Atomiki akijibu swali iwapo kutakuwa na mabadiliko katika ushirikiano wa Iran na IAEA kufuatia maamuzi hayo mapya amesema hakutakuwa na mabadiliko katika ahadi za Iran.

Ameongeza kuwa iwapo pande zingine zitajiondoa katika mapaptano ya nyuklia, basi Iran ina uwezo mkubwa wa kuimarisha shughuli zake za nyuklia.

Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Mei, 2018, rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuitoa nchi yake kwenye mapatano ya JCPOA licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha wakati wa urais wa Barack Obama.

Hatua hiyo ya Marekani imepingwa vikali na nchi zingine zilizo katika mapatano hayo ambazo ni Russia, China, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya.

 

Tags