Rouhani: Iran itajiondoa JCPOA iwapo haitadhaminiwa maslahi yake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45788-rouhani_iran_itajiondoa_jcpoa_iwapo_haitadhaminiwa_maslahi_yake
Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA iwapo itahisi haistafidi wala kupata maslahi yoyote kutokana na mapatano hayo ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 13, 2018 02:45 UTC
  • Rouhani: Iran itajiondoa JCPOA iwapo haitadhaminiwa maslahi yake

Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA iwapo itahisi haistafidi wala kupata maslahi yoyote kutokana na mapatano hayo ya kimataifa.

Rais Rouhani aliyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa hapo jana Jumanne na kuongeza kuwa, "Iwapo Iran haitafaidika na makubaliano hayo, itakuwa muhali kuendelea kubakia kwayo."

Rais wa Iran sambamba na kupongeza taarifa za nchi za Umoja wa Ulaya kuhusu azma ya kuendelea kufungamana na mapatano hayo yanayofahamika kwa kifupi kama JCPOA, ameongeza kuwa, "Tusiruhusu hatua hii kubwa ya kidiplomasia isambatarishwe na hatua za upande mmoja za wakiukaji wa mapatano hayo."

Nchi za Ulaya zinafanya jitihada mbalimbali za kuinusuru JCPOA

Itakumbukwa kuwa Mei 8 mwaka huu, Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuindoa nchi yake kwenye mapatano ya JCPOA licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha wakati wa urais wa Barack Obama.

Nchi zingine tano zilizoafiki mapatano ya JCPOA, zikiwemo za Ulaya zimesisitiza kubakia katika mapatano hayo ya Vienna.

Kwa upande wake, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema nchi yake itaendelea kufugamana na mapatano hayo na kusisitiza kuwa Tehran na Paris zina msimamo mmoja kuhusu kuendelea kutekelezwa na kuheshimiwa makubaliano hayo yaliyosainiwa Julai mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa Januari 2016.