Marekani, Israel, Saudia zinapanga njama za kuudhuri uchumi wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46497-marekani_israel_saudia_zinapanga_njama_za_kuudhuri_uchumi_wa_iran
Marekani, Utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia zinapanga njama za kuzuia na kusitisha mkondo wa ustawi wa uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini hazitafanikiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 01, 2018 09:18 UTC
  • Marekani, Israel, Saudia zinapanga njama za kuudhuri uchumi wa Iran

Marekani, Utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia zinapanga njama za kuzuia na kusitisha mkondo wa ustawi wa uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini hazitafanikiwa.

Hayo yamedokezwa na Eshaq Jahangiri Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Jumapili wakati akihutubu katika sherehe za 'Siku ya Kitaifa ya Viwanda na Madini Iran'. Huku akibainisha kuwa baadhi ya nchi za eneo zinatumiwa vibaya, Jahangiri amongeza kuwa: "Nchi hizo zinaibua matatizo  katika sekta ya fedha za kigeni nchini Iran lakini hatimaye ndizo zitakazodhalilika."

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria njama za Marekani dhidi ya Iran na kusema: "Kusitisha uuzaji wa mafuta ghafi ya petroli ya Iran na kuwasababishia matatizo wale wanaouza mafuta ya Iran kimataifa ni kati ya njama za Marekani zenye lengo la kutoa pigo kwa uchumi wa Iran." Amesema tayari serikali ya Iran imeshachukua hatua zinazohitajika kwa lengo la kukabiliana na njama hiyo.

Jahangiri amesema serikali ya Iran itachukua hatua ambazo zitaifanya Marekani ijute kujaribu kusitisha uuzaji wa mafuta ghafi ya petroli ya Iran katika soko la kimataifa.

Mnamo Mei 8, rais wa Marekani alichukua uamuzi wa upande moja wa kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA. Mapatano hayo yalikuwa yameidhinishwa na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani. Baada ya uamuzi huo, Marekani ilitangaza vikwazo vipya vya nyuklia dhidi ya Iran na imetangaza kuwa kuanzia mwezi Novemba itazuia uuzaji mafuta ya Iran katika soko la kimataifa.