Qassemi: Hakuna msingi wa kuwa na wasiwsi kuhusu makombora ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46740-qassemi_hakuna_msingi_wa_kuwa_na_wasiwsi_kuhusu_makombora_ya_iran
Msemaji wa Wizara ya Nje ya Iran amejibu taarifa iliyotolewa katika kikao cha viongozi wa jumuiya ya kijeshi ya NATO na kusema, hakuna msingi wowote wa kuwa na wasiwasi kuhusu mpango wa makombora ya kujihami ya Iran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 13, 2018 04:11 UTC
  • Qassemi: Hakuna msingi wa kuwa na wasiwsi kuhusu makombora ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Nje ya Iran amejibu taarifa iliyotolewa katika kikao cha viongozi wa jumuiya ya kijeshi ya NATO na kusema, hakuna msingi wowote wa kuwa na wasiwasi kuhusu mpango wa makombora ya kujihami ya Iran.

Bahram Qassemi ameongeza kuwa, taarifa hiyo ya NATO haitakuwa na taathira yoyote katika sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kulinda na kuimarisha uwezo wa mpango wake wa makombora ya kujihami.

Siku ya Jumatano, viongozi wa Muungano wa Kijeshi  wa Atlantiki ya Kaskazini ,kwa kifupi 'NATO' ,katika taarifa yao walidai kuwa na wasiwsi kuhusu hatua za Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na pia mpango wake wa makombora.

Akijibu taarifa hiyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Hakuna shaka kuwa, nchi za NATO zimepata ripoti za mara kwa mara za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kuhusu namna Iran inayavyofungamana na ahadi zake katika kadhia ya nyuklia." Akiashiria hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA, Qassemi amesema badala ya kuwafurahisha watawala wa Marekani, viongozi wa NATO wanapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu kutofungamana Marekani na mapatano hayo ya nyuklia.

Kombora la kujihami la Balisiti la Emad ambalo limeundwa Iran

Qassemi amesema si tu kuwa mpango wa makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayakiuki azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, bali mpango huo ni wa kawaida na wa kujihami. Amesema nchi zote huru duniani zina haki ya kuwa na mpango wa kawaida wa kijeshi na wa kujihami kwa ajili ya kulinda maslahi ya wananchi na nchi.

Qassemi ameashiria kuhusu nafasi chanya ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema: "Iran daima imekuwa ikisisitiza kuhusu kufanyika mazungumzo na nchi jirani katika eneo na haipotezi fursa yoyote katika suala hilo."

Aidha msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema baadhi ya wanachama wa NATO wanaodai kupambana na ugaidi wamehusika katika kuibua au kulea makundi hatari ya kigaidi. Amesema mkabala wa hilo, ni Iran ndio iliyochukua hatua ya kuangamiza makundi hayo ya kigaidi kama vile ISIS ambayo yalikuwa yameteka ardhi za nchi za eneo.