Qassemi: Yaliyozungumzwa baina Mjumbe wa Iran na Rais wa Russia hayajatangazwa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Yaliyozungumzwa baina ya Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa na Rais Vladimir Putin wa Russia hayjatangazwa."
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akizungumza na waandishi habari Jumatatu mjini Tehran ameashiria mkutano uliofanyika baina ya Ali Akbar Velayati, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Rais Vladimir Putin wa Russia Alhamisi iliyipita mjini Moscow na kusema, mkutano huo hauna uhusiano wowote na mkutano wa leo baina ya Putin na Rais wa Marekani mjini Helsiniki, Finland.
Amongeza kuwa mkutano huo wa Helsiniki hauhusiani na Iran na pia Iran haijamtumia ujumbe wowote Rais Donald Trump wa Marekani. Qassemi pia ametupilia mbali madai aliyoyataja kuwa ni kichekeso kuwa eti Russia ni mpatanishi baina ya Iran na utawala haramu wa Israel.

Qassemi ameongeza kuwa, yaliyotajwa katika vyombo vya habari kuhusu yaliyojadiliwa katika mkutano wa masaa mawili baina ya Putin na Velayati ni machache mno na kwamba masuala muhimu yaliyojadiliwa hayakutangazwa.
Amesema Velayati alifika Russia kama mjumbe maalumu wa Rais wa Iran na pia alikuwa na ujumbe maalumu kutoka kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Rais Putin.
Akijibu swali la iwapo Iran itabakia au itaondoka katika mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA, Qassemi amesema: "Baada ya Marekani kujiondoa kinyume cha sheria katika JCPOA, nchi za Ulaya na hata China na Russia zinaamini kuwa, mapatano hayo ya kimataifa yanapaswa kulindwa sambamba na kuwasilishwa njia za kuifanya Iran inufaike na mapatano hayo."
Aidha amesema nchi za Ulaya, Russia na China zinapaswa kuchukua hatua za haraka kudhamini maslahi ya Iran katika JCPOA.