Ayatullah Movahhedi Kermani: Jeshi la Kiislamu liliwasambaratisha wanafiki katika operesheni ya 'Mirsad'
Ayatukllah Muhammad Ali Movahhedi Kermani, Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, kundi la kigaidi la Munafiqin lilikuwa likitaka kuidhibiti Iran na kuuangusha mfumo wa kiislamu hapa nchini, lakini operesheni kubwa ya kijeshi iliyopewa jina la "Mirsad" ililisambaratisha kundi hilo.
Kundi la Munafiqin ambalo lilikuwa limekusanya magaidi katika mpaka wa Iran na Iraq wakiwa na silaha nzito kutoka kwa utawala wa zamani wa Baghdad lilianza kuishambulia ardhi ya Iran siku mbili kabla ya kuanza operesheni hiyo.
Kiongozi wa Munafiqin alidhani kuwa magaidi hao wangeweza kuvuka barabara kuu za Iran bila ya kizuizi na tabu yoyote na kufika haraka mjini Tehran. Hata hivyo wanajeshi wa Iran wakishirikiana na wananchi waliojitolea katika operesheni hiyo ya Mirsad waliwazingira vibaraka hao wa Munafiqin huko magharibi mwa nchi na kuwasambaratisha magaidi hao walio na uhusiano mkubwa na nchi za kigeni.
Zaidi ya wapiganaji 2,000 wa kundi la kigaidi la Munafiqin waliangamizwa katika operesheni hiyo kubwa iliyopewa jina la 'Mirsad'.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake ya Swala ya Ijumaa mjini Tehran, Ayatullah Movahhedi Kermani, amezungumzia matatizo ya kiuchumi hapa nchini na kuitaka serikali ichukue hatua za maana na madhubuti kwa ajili ya kulishughulikia tatizo hili.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa hapa Tehran amesema kuwa, serikali inapaswa kuwa na sauti moja ya kiuchumi na wakati huo huo kuwatumia vijana amilifu na wenye vipawa katika suala zima la kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kiuchumi.