Zarif: Marekani "imeyakejeli" matakwa ya kutaka amani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, serikali ya Marekani imeyafanyia kejeli matakwa ya amani.
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter katika radiamali yake kwa matamshi ya Brian Hook, Mkuu wa "Kundi la Kuchukua Hatua Dhidi ya Iran" katika Wizara ya Mashauuri ya Kigeni ya Marekani na kuongeza kuwa: Marekani imeyataja makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kama 'makubaliano binafsi baina ya madola mawili' na kudai kwamba, hivi sasa inafuatilia 'mkataba maalumu', kwa hakika madai haya si sahihi kabisa.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameyataja makubaliano ya JCPOA kuwa ni makubaliano ya kimataifa ambayo yamethibitishwa na kuungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, Marekani imekiuka ahadi na majukumu yake katika makubaliano hayo.
Brian Hook, Mkuu wa "Kundi la Kuchukua Hatua Dhidi ya Iran" katika Wizara ya Mashauuri ya Kigeni ya Marekani alidai siku ya Jumatano kwamba, JCPOA ni makubaliano binafsi baina ya serikali ya Iran na Barack Obama Rais aliyepita wa Marekani na kusema kuwa, hivi sasa Washington inafuatilia kuwa na mkataba maalumu na Iran ambao utadhibiti mpango wa makombora pamoja na miradi ya nyuklia ya Tehran.
Dakta Zarif amesisitiza kwamba, inaonekana Marekani inayakebehi matakwa ya walimwengu ya kutaka amani, je haioni hata haya katika hilo?