Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; kupatiwa ufumbuzi matatizo ya kiuchumi kwa kuweko ushirikiano
(last modified Fri, 12 Oct 2018 07:58:11 GMT )
Oct 12, 2018 07:58 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; kupatiwa ufumbuzi matatizo ya kiuchumi kwa kuweko ushirikiano

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza katika mazungumzo yake na wakuu wa mihimili mikuu mitatu ya dola kuhusiana na masuala ya uchumi kwamba, matatizo ya kiuchumi hapa nchini yanatokana na changamoto za ndani na muundo wa kiuchumi hapa nchini huku matatizo mengine yakisababishwa na vikwazo vya kidhulma vya Marekani.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, akiwahutubu wakuu wa mihimili mikuu mitatu ya dola yaani Serikali, Bunge na Idara ya Mahakama juzi Jumatano alisema bayana kwamba: Tumieni mbinu na ufumbuzi wa busara ambapo natija yake itakuwa ni utatuzi wa kudumu na endelevu wa maisha ya watu na kumkatisha tamaa adui kwa kutokuwa na taathira wenzo na silaha yake ya vikwazo.

Masuala ya uchumi hii leo ni daghadagha na hangaiko la nchi mbalimbali ulimwenguni, na Iran nayo inakabiliwa na tatizo hili. Sehemu ya matatizo ya kiuchumi ya Iran chimbuko lake ni muundo wa uchumi huku sehemu nyingine ya matatizo hayo chimbuko lake likiwa ni sera za Marekani za kuyawekea vikwazo mataifa mengine.

Wakuu wa mihimili mikuu mitatu ya dola: Rais Hassan Rouhani (katikati), Spika wa Bunge Ali Larijani (kulia) na Mkuu wa  Vyombo vya Mahakama Ayatullah Sadiq Amoli Larijani (kushoto)

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini sera za kuiwekea vikwazo Iran zilifanywa kuwa miongoni mwa ajenda za serikali ya Marekani, na hivi sasa sera hizo zimeshadidishwa na serikali ya sasa ya Washington chini ya uongozi wa Rais Donald Trump. Historia ya miaka 40 ya uhai wa Mapinduzi ya Kiislamu inaonyesha kuwa,  hakuna kitu kinachoitwa mkwamo nchini Iran; na ni kwa sababu hiyo ndio maana mapinduzi haya yanapiga hatua mbele na yamo katika kujipatia ustawi na maendeleo siku baada ya siku.

Serikali ya Rais Donald Trump inafanya njama za kushadidisha vikwazo ili kuifanya Iran ielekee katika mkondo inaotaka Washington. Hata hivyo serikali na wananchi wa Iran wamefanikiwa kuvuka salama na kwa wakati unaotakiwa kipindi kigumu kabisa kwa ushirikiano na umoja. Katika uwanja huo, Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Oktoba Pili  mwezi huu sambamba na kubainisha kwamba, Trump akiwa na malengo ya kisiasa amechukua hatua kwa jina la 'vita vya kiuchumi' akitumia wenzo wa vikwazo pamoja na propaganda ili kutoa pigo kwa Iran na kusema kuwa, Marekani inataka kutoa pigo dhidi ya uchumi, usalama na nafasi ya kieneo ya Iran, lakini Iran inavichukulia vitisho hivyo kuwa ni fursa.

Vikkwazo vya Marekani dhidi ya Iran

Sambamba na kushadidi sera na siasa za vikwazo za Marekani, viongozi wa Iran wameandaa mipango na mikakati mbalimbali ambapo sanjari na kufubaza na kudhoofisha wenzo wa vikwazo vya Marekani na kurekebisha muundo wa uchumi, wahakikishe kwamba, kunakuweko na madhara madogo sana kwa wananchi hususan wa tabaka la chini. Panda shuka inayoshuhudiwa hivi sasa katika soko la ubadilishaji fedha za kigeni, kuongezeka bei ya baadhi ya bidhaa na kupungua uwezo wa wananchi kufanya manunuzi hususan tabaka la kipato cha chini, limeifanya serikali kufanya juhudi maradufu na kuwa na ushirikiano baina ya viongozi husika katika sekta mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, matatizo yaliyopo yanapatiwa ufumbuzi.

Katika fremu hiyo, kumekuwa kukifanyika kikao takribani kila wiki cha Baraza Kuu la Uratibu wa Uchumi kwa kuhudhuriwa na viongozi wa mihimili mikuu mitatu ya dola lengo hasa likiwa ni kuandaa mipango ya lazima ya kusukuma mbele gurudumu la sera za kiuchumi.

Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuwa,  kuweko ushirikiano wa mihimili mikuu mitatu ya dola na vyombo vingine tofauti sambamba na kutumiwa ipasavyo uwezo usio na mbadala wa vijana wa Kiirani, wenye vipawa na kuufanya kuwa na harakati amilifu uwezo uliopo na rasilimali bora ni mambo ambayo yanaweza kusaidia kuyashinda matatizo ya ndani na ya kutwishwa yaliyoko hivi sasa hapa nchini.

Abdolnaser Hemmati, Gavana wa Benki Kuu ya Iran

Katika uga wa ndani, Iran kutokana na kuwa na rasilimali na vyanzo vingi vya utajiri na kupiga hatua kubwa katika uwanja wa teknolojia ya nano na elimu nyingine mpya, inaweza kuwa na aina kwa aina ya sekta za kujipatia kipato na hivyo kupunguza utegemezi kwa mafuta na kuathirika katika uwanja huo kutokana na vikwazo vya Marekani. Katika upande wa matatizo ya kutwishwa, vile vile  inawezekana kuzikwamisha sera za vikwazo za Marekani na kuzifanya zisiwe na taathira hasi kwa uchumi wa Iran kama tajiriba ya huko nyuma inavyoonyesha. Hilo linawezekana kupitia ushirikiano wa pamoja wa wakuu wa mihimili mikuu mitatu ya dola sambamba na wananchi na hivyo kukabiliana na tamaa na siasa za kupenda makuu za Washington.

Katika uwanja huo,  Abdolnaser Hemmati , Gavana wa Benki Kuu ya Iran sambamba na kubainisha kwamba, Marekani inafanya kazi usiku na mchana ili  kukwamisha harakati za kifedha na uuzwaji mafuta ya Iran nje ya nchi ameeleza kuwa,  Wamarekani hawajafanikiwa katika kuleta taathira hasi kwa uchumi wa Iran na hawajaweza kufanikiwa pia katika kubinya mabadilishano ya fedha na uuzwaji mafuta ya Iran na hakuna njia na mazingira ya kuwafanya wafanikiwe katika hilo.