Iran: Ushindi wa Trump hautakuwa na athari yoyote kwa uchumi wetu
Gavana wa Benki Kuu ya Iran (CBI), Mohammad-Reza Farzin amesema kuchaguliwa tena Donald Trump kuwa rais wa Marekani hakuna mfungamano wowote na ustawi wa uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu.
Farzin alisema katika mahojiano ya televisheni jana usiku na kuongeza kuwa, "Trump kama rais hana athari za moja kwa moja kwa uchumi wa Iran kwa sababu hatuna ushirikiano wowote wa moja kwa moja wa kibiashara, kimuamala na kifedha na Marekani au hata Ulaya."
Mkuu huyo wa CBI, hata hivyo, amebainisha kuwa, uchumi wa kimataifa na masoko ya fedha yanaweza kuhisi joto iwapo sera itabadilika na utawala unaokuja wa Marekani.
Kwa upande wa ndani, Mkuu wa Benki Kuu ya Iran ameonyesha matumaini kwamba, mfumuko wa bei wa nchi utapungua hadi kiwango cha asilimia 30 kufikia mwishoni mwa mwaka, na kisha hadi 20%.
Hivi karibuni pia, Rais wa Iran alisema: Haijalishi kwa Jamhuri ya Kiislamu ni nani ameshinda uchaguzi wa rais nchini Marekani.
Rais Masoud Pezeshkian amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni taifa lenye heshima na adhimu linaloegemea kwenye nguvu zake za ndani.
Alisema, kwa Iran hakuna tofauti nani ameshinda uchaguzi wa rais huko Marekani, kwa sababu Iran na muundo wa Jamhuri ya Kiislamu unategemea nguvu zake za ndani.