Sep 01, 2024 07:22 UTC
  • Pezeshkian: Umoja ndio njia bora ya kukabiliana na matatizo ya kiuchumi

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesisitiza haja ya kulinda umoja wa kitaifa miongoni mwa mirengo na makundi mbalimbali ya kisiasa ili kuwatumikia vyema zaidi wananchi.

Akilihutubia taifa mubashara kwa njia ya televisheni jana usiku kwa mara ya kwanza baada ya kula kiapo cha urais karibu mwezi mmoja uliopita, Dakta Pezeshkian amesisitiza kuwa, umoja ndiyo njia bora zaidi ya kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazoikabili nchi.

Amebainisha kuwa, "Hadi sasa, tumefanya juhudi kubwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, baraza langu la mawaziri la muafaka wa kitaifa linajumuisha shakhsia kutoka serikali ya zamani ya Shahidi Ebrahim Raisi, mtangulizi wake Hassan Rouhani na wanamageuzi."

Rais Pezeshkian ameufungamanisha uchumi na sera ya mambo ya nje na kusema kuwa, mashirikiano na biashara na nchi jirani na dunia nzima ni njia ya kutatua matatizo ya kiuchumi, akisema kuwa mipango inahitajika kufanywa kuvutia wawekezaji wa kigeni.

Dkt Pezeshkian katika mahojiano na wanahabari wa Kanali ya 1 ya Iran

Rais wa Iran amebainisha kuwa, ili kufikia ukuaji wa uchumi kwa asilimia 8, dola bilioni 100 zinafaa kuvutiwa kutoka ndani na nje ya nchi.

Dakta Pezeshkian ameongeza kuwa: Ninaamini kuwa, hivi sasa tunapaswa kushikana mikono na kusonga mbele kwa umoja. Aidha ameashiria ahadi yake ya kuwa mwaminifu kwa watu na kusisitiza kuwa atafanya kila awezalo kutatua matatizo ya nchi.

 

Tags