Zarif: Iran inapigania eneo lenye nguvu na lenye ushirikiano wa wote
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, siasa za Tehran zimesimama juu ya msingi wa kushirikiana vizuri na majirani zake na kwamba kinachopiganiwa na Iran ni kuweko eneo lenye nguvu na lenye ushirikiano wa wote.
Dk Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika mahojiano yaliyochapishwa leo Jumatatu na gazeti la al Wifaq na kusisitiza kuwa, baadhi ya nchi za nje ya eneo hili zinafanya njama za kuainisha siasa za eneo la magharibi mwa Asia. Vile vile amesema, inasikitisha kuona baadhi ya nchi za eneo hili, zinafikiria kushirikiana na madola ajinabi kwa madhara ya ushirikiano wa nchi za eneo hili. Amesisitiza kuwa, ushirikiano wa kiusalama wa nchi za eneo hili na madola ajinabi ya kibeberu umefeli na hauna matunda yoyote isipokuwa kuhatarisha tu usalama wa nchi za magharibi mwa Asia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amezungumzia mgogoro wa Yemen na kusema kuwa, tangu mwanzoni kabisa mwa uvamizi wa Saudi Arabia huko Yemen, Iran ilitoa pendekezo la vipengee vinne ambavyo ni kusimamishwa vita haraka, kupelekwa misaada ya kibinadamu, kufunguliwa milango ya mazungumzo baina ya Wayemen wenyewe kwa wenyewe na kuundwa serikali kubwa itakayoshirikisha mirengo yote nchini humo, lakini cha kusikitisha ni kuwa, baadhi ya nchi zilianza kuendesha propaganda mbaya dhidi ya Iran na leo hii tunaona madhara ya uvamizi huo wa Yemen.
Aidha amesema, hadi hivi sasa Iran inaamini kuwa migogoro ya Yemen na Syria haiwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi, bali ni mazungumzo tu ndiyo yatakayotatua migogoro hiyo.
Amma kuhusu mfumo wa kubadilishana fedha baina ya Iran na Ulaya maarufu kwa jina la SPV, Zarif amesema, nchi za Ulaya zinapaswa kugharamia mustakbali na uhuru wao na zisidhani kuwa kila kitu kitagharamiwa na Iran.