Rais Rouhani: Marekani inatiwa kiwewe na ustawi na maendeleo ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50916-rais_rouhani_marekani_inatiwa_kiwewe_na_ustawi_na_maendeleo_ya_iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Wamarekani wameamua kuliwekea taifa la Iran vikwazo vikubwa mno kwa sababu wana kiwewe na maendeleo, ustawi na uwezo wa taifa hili la Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 16, 2019 12:01 UTC
  • Rais Rouhani: Marekani inatiwa kiwewe na ustawi na maendeleo ya Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Wamarekani wameamua kuliwekea taifa la Iran vikwazo vikubwa mno kwa sababu wana kiwewe na maendeleo, ustawi na uwezo wa taifa hili la Kiislamu.

Rais Rouhani amesema hayo leo Jumatano katika kikao cha pamoja cha Baraza la Mawaziri na Wakuu wa Mikoa yote ya Iran na kuongeza kuwa, Wamarekani sasa hivi wameliwekea taifa la Iran vikwazo vikubwa mno kwa kushirikiana na vibaraka wake, lakini kwa ushirikiano mzuri uliopo baina ya wananchi na serikali ya Iran, njama hizo zote zimefeli.

Vile vile ametilia mkazo wajibu wa kustawishwa ushirikiano wa Iran na majirani zake na kusisitiza kwamba, sekta binafsi ya Iran ina uhusiano mzuri na wa karibu na sekta binafsi za nchi nyingine hususan majirani wa Iran na kwamba ushirikiano huo utaendelea kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.

Iran yakandamiza vikwazo vya Marekani

 

Aidha amesema kuwa, sekta ya usafirishaji na uchukuzi ya Iran imechukua hatua nzuri za kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine na kukumbusha kuwa, hivi sasa sekta ya meli za kuvuka mabara za Iran imeongeza meli nyingine 10 katika safari zake za kuzunguka dunia.

Rais Rouhani amezungumzia pia satalaiti iliyorushwa jana na Iran katika anga za juu na kuongeza kuwa, Iran imepiga hatua kubwa katika mchakato mzima wa utengenezaji wa satalaiti na kuzirusha anga za mbali.

Katika ujumbe wake kupitia Twitter, Mohammad Javad Azari Jahromi Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran alitangaza jana Jumanne habari ya kurushwa katika anga za mbali satalaiti hiyo iliyoundwa na wahandisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Alisema satalaiti hiyo iliweza kuvuka awamu ya kwanza na ya pili lakini kutokana na kukosekana kasi ya kutosha haikuweza kufika katika nukta iliyotakiwa ili kuzunguka sayari ya dunia.  Waziri Jahromi amesema Iran itaendeleza kwa nguvu zake zote mpango wake wa kuunda na kurusha satalaiti katika anga za mbali.