Zarif: Iran inaliunga mkono taifa la Venezuela dhidi ya njama za Marekani
(last modified Sat, 26 Jan 2019 04:37:38 GMT )
Jan 26, 2019 04:37 UTC
  • Zarif: Iran inaliunga mkono taifa la Venezuela dhidi ya njama za Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kulaani uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela, amesema Iran inaliunga mkono taifa hilo la Amerika ya Latini na itasimama nalo dhidi njama ya mapinduzi inayopikwa na Marekani.

Katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Venezuela, Jorge Arreaza, Dakta Mohammad Javad Zarif amesema Iran inaiunga mkono serikali halali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Nicolás Maduro na ambayo imechaguliwa kidemokrasia.

Wawili hao pia wamebadilishana mawazo kuhusu njia zinazoweza kutumika kuzima njama hizo haribifu za Marekani sanjari na kuupatia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro unaoikabili nchi hiyo kwa sasa, kwa kutumia taasisi za kimataifa.

Kabla ya hapo, Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema kuwa Tehran inalaani uingiliaji wowote wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Venezuela na inakihesabu kitendo chochote kilicho kinyume cha katiba kuwa ni sawa na mapinduzi dhidi ya wananchi, serikali na taifa hilo zima la Amerika ya Latini.

Rais Nicolás Maduro wa Venezuela

Nchi nyingine mbalimbali duniani kama vile Russia, Uturuki na Iran zimeendelea kulaani uingiliaji huo wa masuala ya ndani ya Venezuela unaofanywa na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani.

Mgogoro mpya umezuka nchini Venezuela baada ya Juan Guaido, spika wa bunge aliyefutwa kazi, kujitangazia urais wa nchi hiyo. Marekani ilikuwa nchi ya kwanza kabisa kumtambua rasmi Guaido licha ya kwamba ni kiongozi wa waasi ambaye amekwenda kinyume kabisa na katiba ya Venezuela. 

Tags