Onyo la Iran kwa chokochoko za Israel dhidi ya Syria
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa nchini Iran ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kuendelea kuishambulia Syria.
Ali Shamkhani alitoa tahadhari hiyo hapo jana katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Walid Muallem, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria na kuongeza kuwa, hatua zozote za kichokozi za Israel dhidi ya Syria hazikubaliki.
Amebainisha kuwa, hatari ya ugaidi na mizizi yake ni miongoni mwa fikra za kitakfiri zinazoenezwa na baadhi ya nchi za Kiislamu katika Mashariki ya Kati ambazo zimelitumbukiza eneo lote hili katika mgogoro na kuwa kikwazo kikubwa katika njia ya ustawi na maendeleo ya nchi za Kiislamu.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuna ulazima wa kuwa macho, kuongeza ushirikiano na mazungumzo kwa shabaha ya kukwamisha na kusambaratisha njama haribifu za wale wenye kuyatakia mabaya mataifa ya Kiislamu na ambao wanafanya kila wawezalo ili kuleta mtazamo mbaya na kuzusha hitalafu baina ya nchi za eneo, haswa Marekani na utawala wa Kizayuni.
Naye Walid Muallem, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema serikali ya Damascus itaendelea kufanya mazungumzo na makundi ya wapinzani ambayo hayabebi silaha, yenye nia ya kulinda uhuru wa kujitawala nchi hiyo ya Syria.
Haya yanajiri siku chache baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya mashambulizi ya makombora ukilenga mji mkuu wa Syria, Damascus. Hata hivyo mfumo wa ulinzi wa anga wa Syria ulitungua makombora hayo ya Israel.